Home Kitaifa ASASI ZA KIRAIA ZATAKIWA KUSHIRIKIANA NA MAWAKILI KUTETEA HAKI ZA WANANCHI

ASASI ZA KIRAIA ZATAKIWA KUSHIRIKIANA NA MAWAKILI KUTETEA HAKI ZA WANANCHI

Celebrating 25 Years of NHIF
ASASI ZA KIRAIA ZATAKIWA KUSHIRIKIANA NA MAWAKILI KUTETEA HAKI ZA WANANCHI

Asasi za kiraia nchini zimehimizwa kuimarisha ushirikiano na mawakili ili kuongeza nguvu katika kutetea haki za wananchi, kushughulikia changamoto za kisheria na kushawishi maboresho ya mifumo inayokwamisha upatikanaji wa haki katika jamii.

Wito huo umetolewa leo Novemba 23,2026 jijini Dodoma kupitia mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), yaliyowakutanisha zaidi ya washiriki 30 kutoka asasi za kiraia na Chama cha Wanasheria (Bar Association).

FAHARI AFYA

Akizungumza kando na mafunzo hayo Wakili na Mkuu wa Idara ya Utetezi kutoka THRDC Paul Kisabo, amesema asasi za kiraia zinafanya kazi moja kwa moja na wananchi hivyo zinahitaji kuwa na ujuzi wa kutambua changamoto, kuzichambua na kushirikiana na taasisi zinazohusika kutafuta suluhisho.

“Watetezi wa haki za binadamu wanakutana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao zikiwemo zinazohusiana na baadhi ya sheria kuhusu makosa ya mtandao (Cybercrimes Act), uhuru wa kujieleza na madai ya uchochezi,”amesema.

Aidha, Wakili Kisabo ametolea mfano changamoto za ustawi wa wafungwa na mahabusu akisema baadhi yao wanahitaji huduma na vifaa maalumu vinavyohusiana na hali zao lakini upatikanaji wake unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wadau na mamlaka za magereza.

Ametaja mahitaji ya viti mwendo kwa wafungwa wenye ulemavu na mafuta ya kujikinga na mionzi ya jua kwa watu wenye ualbino ili kupunguza hatari ya madhara ya ngozi, yakiwemo saratani.

Kwa upande wake, Wakili na Mkurugenzi wa Msasa Law Chamber Thomas Msasa amesema mafunzo hayo yamewapa washiriki uelewa wa namna ya kutumia ushahidi na tafiti katika kuibua changamoto za jamii na kuzifikisha kwa Serikali kwa hoja zenye msingi.

“Uchechemuzi wenye tija unapaswa kuanzia katika kubaini tatizo, kulifanyia utafiti na kuthibitisha ukubwa wake kabla ya kuishirikisha Serikali au mamlaka husika ili kupata hatua zinazoweza kutekelezeka,”amesema.

Akieleza baadhi ya changamoto zinazohitaji maboresho ya kisheria Wakili Msasa amesema wananchi wanaoshinda kesi dhidi ya Serikali wakati mwingine hukumbana na ucheleweshaji wa utekelezaji wa hukumu zinazowaamuru kulipwa fidia.

Naye, Mwakilishi wa Kaya Foundation Bi. Anna Ngome, amesema shirika hilo linalofanya kazi na watoto wenye ulemavu na wanawake pamoja na kutoa msaada wa kisheria linatarajia kutumia maarifa yaliyopatikana kuimarisha ushirikiano na mawakili pamoja na Serikali.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza ufanisi wa shughuli za asasi za kiraia na kuhakikisha changamoto zinazohitaji uamuzi wa kisheria au kisera zinafikishwa katika mamlaka zinazoweza kuzitatua.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea washiriki uwezo katika masuala ya uchechemuzi (advocacy), ushirikishwaji wa taasisi mbalimbali (engagement) na utawala wa sheria ili kuboresha namna wanavyoshughulikia changamoto za wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!