Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema kuwa pamoja na kuhakikisha Ugonjwa wa Ebola hauingii nchini, pia imejipanga kuhakikisha kwamba mgonjwa akipatikana nchini anatibiwa bila kusababisha maambikizi kusambaa.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Mratibu Shughuli za Kukinga na Kudhibiti maambikizi Nchini kutoka Wizara ya Afya, Joseph Christopher Hokororo, wakati akitoa mafunzo kwa Wanahabari jinsi ya kujikinga na Ugonjwa wa Ebola.
“Sasa hivi maelekezo ni kwamba kila halmashauri iwe na sehemu ambayo imetenga iwapo mgonjwa atapatikana katika halmashauri husika kuwepo na sehemu ya kutibu mgonjwa. Serikali imeandaa vifaa mbalimbali, vifaa vya kinga binafsi kwa ajili ya wataalamu wetu, dawa na inaendelea kutoa elimu kwa watoa huduma wetu na kuwajengea uwezo watoa huduma wetu kwa mkoa wa Dar es Salaam zaidi ya Elfu Tatu ambao janga likitokea tunaweza kuwapeleka sehemu yoyote na kuendelea kutoa huduma“

Hata hivyo amesema, vijidudu vya Ebola vikiingia mwilini jambo la kwanza ambalo huwa vinaenda kufanya ni kushambulia kinga mwili.
“Baada ya hapo vinakuacha ukiwa hauna kinga yoyote mwilini, hivyo ndiyo maana tunashauri kila mmoja achukue tahadhari na pale ambapo anaona dalili za ugonjwa huo achukue hatua za haraka kuripoti kituo cha afya,”amesema Dkt.Hokororo.
Aidha amesema katika ya jamii na maofisini kuendelea kutumia maji tiririka na sabuni ili kupunguza uwezekano wakupata maambukizi
“unawaji wa mikono na sabuni ni kinga muhimu sana na inazuia magonjwa mengi mpaka asilimia tisini unauhakika wa kuwa salama, vijidudu vingi vinaaribiwa na sabuni” amesema Dkt.Hokororo.
Hata hivyo Dkt.Hokororo ameitaka jamii kuendelea kufuata taratibu na miongozo ya afya inawezesha kuepusha mtu kuepukana na magonjwa ya milipuko kama vile Ebola au Corona.








