Home Kitaifa Tbs Kuhakikisha Magari Na Mabasi Yanayotumika Nchini Yanakidhi Viwango Vya Ubora Na...

Tbs Kuhakikisha Magari Na Mabasi Yanayotumika Nchini Yanakidhi Viwango Vya Ubora Na Usalama

Celebrating 25 Years of NHIF

DAR ES SALAAM: Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau wa sekta ya usafiri wa ardhini kuhusu umuhimu wa viwango vya ubora na usalama wa vyombo vya usafiri, katika Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2026 yanayofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

FAHARI AFYA

Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi pamoja na wadau mbalimbali, yanafanyika kuanzia Novemba 24 hadi 26, 2026, yakiwa na kaulimbiu isemayo “Kuharakisha Usafiri Endelevu: Usafiri Salama, Rafiki kwa Mazingira na Jumuishi.“

Katika maonesho hayo, TBS imepata fursa ya kutoa elimu kwa wananchi na wadau waliotembelea banda lake kuhusu majukumu ya taasisi hiyo katika kuandaa viwango vya vyombo mbalimbali vya usafiri, ikiwemo magari ya abiria, magari binafsi, magari makubwa na madogo, bajaji pamoja na pikipiki.

Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Masoko Mwandamizi wa TBS, Deborah Haule, amesema kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kuandaa viwango vinavyolenga kuhakikisha vyombo vya usafiri vinavyotumika nchini vinakidhi matakwa ya ubora na usalama.

Amesema kuwa baada ya kuandaa viwango hivyo, TBS pia husimamia utekelezaji wake kupitia mifumo mbalimbali ya ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini.

Ameeleza kuwa mifumo hiyo ni pamoja na ukaguzi wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuingia nchini, unaojulikana kama Pre-Shipment Verification of Conformity (PVoC), pamoja na ukaguzi wa bidhaa baada ya kuwasili nchini, unaojulikana kama Destination Inspection (DI).

Kwa mujibu wa Haule, mifumo hiyo inalenga kuhakikisha magari na bidhaa nyingine zinazoingizwa nchini zinakidhi matakwa ya viwango husika, hatua inayosaidia kuzuia bidhaa zisizokidhi ubora na usalama kuingia katika soko la Tanzania.

Aidha, amesema TBS inaandaa kiwango kinachohusu madaraja ya huduma za mabasi ya abiria, ambapo mabasi yanaainishwa kulingana na aina ya huduma zinazotolewa, ikiwemo Ordinary, Semi-Luxury na Luxury.

Ameeleza kuwa uwepo wa kiwango hicho utasaidia kuwawezesha abiria na wamiliki wa mabasi kutambua tofauti za madaraja ya huduma zinazotolewa, hivyo kuongeza uelewa na uwazi katika sekta ya usafiri wa abiria.

Katika hatua nyingine, Haule amesema TBS pia inaandaa kiwango kinachohusu udhibiti wa mwendo wa mabasi, kwa lengo la kuhakikisha mabasi yanafuata matakwa yaliyowekwa kuhusu mwendo wakati wa safari.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha usalama barabarani, kupunguza uwezekano wa kutokea kwa ajali na kulinda maisha ya abiria pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

Ushiriki wa TBS katika maadhimisho hayo ni sehemu muhimu ya kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu nafasi ya viwango katika kujenga mfumo wa usafiri ulio salama, bora na endelevu.

Kupitia elimu inayotolewa katika banda lake, TBS imeendelea kuwafikia wadau wa sekta ya usafiri na wananchi kwa ujumla, ikiwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango katika vyombo vya usafiri na bidhaa nyingine zinazotumika katika maisha ya kila siku.

Kwa ujumla, ushiriki wa TBS katika Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2026 unaonesha umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi za serikali na wadau mbalimbali katika kuhakikisha sekta ya usafiri inakuwa salama, bora, rafiki kwa mazingira na yenye kuzingatia mahitaji ya wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!