Na.Alex Sonna–DODOMA
WATAALAMU wa afya ya mazingira nchini wametakiwa kuimarisha utayari na mikakati ya kukabiliana na majanga ya kiafya yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa za El Niño, milipuko ya magonjwa na changamoto nyingine za kimazingira zinazoweza kuhatarisha afya za wananchi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Mazingira na Usafi kutoka Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Dkt. Amour Seleman, wakati Kongamano la Usafi wa Mazingira lililoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Choo Bora Duniani jijini Dodoma lililowakutanisha maafisa afya wa mikoa na wilaya, wakuu wa vitengo vya usafi na udhibiti wa taka pamoja na watumishi wa afya mipakani, kwa lengo la kujadili utendaji na kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na changamoto za afya ya jamii.
Dkt. Seleman amesema kikao hicho kilikuwa muhimu katika kuwakumbusha wataalamu hao kuhusu matishio mbalimbali yanayoikabili sekta ya afya, ikiwemo uwezekano wa kutokea kwa mafuriko na milipuko ya magonjwa kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha katika baadhi ya maeneo nchini, akisisitiza umuhimu wa kuwa na maandalizi ya mapema badala ya kusubiri majanga yatokee.
Katika hatua nyingine, Dkt. Seleman amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usafi wa mazingira katika miji na maeneo mbalimbali nchini, akieleza kuwa maandalizi hayo ni muhimu zaidi kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ambapo mazingira safi yatakuwa sehemu ya taswira ya nchi mbele ya wageni na washiriki watakaotembelea maeneo mbalimbali.
Amesema katika kikao hicho wataalamu wamejadili changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo upungufu wa miongozo, udhaifu wa mifumo ya kitaasisi na ukosefu wa motisha kwa baadhi ya watumishi, huku akibainisha kuwa maazimio yaliyofikiwa yanapaswa kuwa msingi wa kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi katika kusimamia usafi wa mazingira.
“Wataalamu wanapaswa kutumia ipasavyo sheria, kanuni na zana za kazi zilizopo katika kutekeleza majukumu yao, huku akiwataka kutokaa kimya wanapokutana na changamoto bali kuzifikisha katika mamlaka husika kwa wakati, akionya kuwa katika kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia taarifa za changamoto za kiutendaji zinaweza kusambaa haraka na kufikishwa katika ngazi za juu kabla hazijashughulikiwa.“amesema Dkt. Seleman
Dkt. Seleman amesisitiza kuwa maazimio yaliyotokana na kikao hicho ni matokeo muhimu ya majadiliano ya siku mbili, hivyo amewataka washiriki kuhakikisha yanatekelezwa kwa vitendo ili kuimarisha huduma za afya ya mazingira, kulinda afya za wananchi na kuweka miji katika hali ya usafi na usalama.
Aidha ameeleza kuwa Wizara itaendelea kuweka mazingira ya kukutana kwa wigo mpana zaidi ili kuwashirikisha wadau wengi wa afya ya mazingira katika kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Sehemu ya Afya na Usafi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Seleman Yondo, amesema kikao hicho kimekuwa jukwaa muhimu la kujadili masuala ya kitaifa, kujifunza jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na kubadilishana uzoefu kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za afya ya mazingira.
“Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI iko tayari kusimamia utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho katika ngazi za mikoa na halmashauri, huku akisisitiza umuhimu wa kuweka mifumo ya ufuatiliaji na utoaji wa mrejesho ili kuhakikisha maazimio hayo yanatekelezwa kikamilifu.“amesema Bw.Yondo
Aidha, amewataka maafisa afya wa mikoa na halmashauri kuandaa muhtasari wa maazimio na kuyawasilisha kwa viongozi na menejimenti zao ili maelekezo yashushwe hadi ngazi za kata, vijiji na mitaa kwa ajili ya utekelezaji, akisisitiza kuwa mifumo ya Serikali za Mitaa inapaswa kuwajibika katika kusimamia usafi wa mazingira, ujenzi bora na ufuatiliaji wa viashiria vya magonjwa katika maeneo yao.

Naye Msajili wa Baraza la Wataalamu wa Afya ya Mazingira Tanzania kutoka Wizara ya Afya, John Kijumbe, amewataka wataalamu wa afya ya mazingira nchini kuzingatia sheria, nidhamu, weledi na maadili ya taaluma katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma wanazozitoa kwa wananchi.
Kijumbe amewakumbusha wataalamu hao kuhakikisha wanakamilisha usajili na kuhuisha leseni zao za utendaji, akisisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria, usajili na kuwa na leseni hai ni takwa la lazima na si hiari.
Aidha, amewataka kusimamia ubora wa huduma zinazotolewa na taasisi zinazohusika na afya ya mazingira, zikiwemo huduma za majitaka, taka ngumu na uendeshaji wa mitambo ya kuteketeza taka , ili kuhakikisha zinakidhi matakwa ya sheria na viwango vinavyotakiwa.
Katika hatua nyingine, amewataka wataalamu wenye uzoefu kusimamia kwa karibu wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo ili kuwajengea uwezo wa kutosha kabla ya kuingia katika soko la ajira.
Pia amewahimiza kutoa taarifa Baraza kuhusu vyuo vinavyotangaza kozi za afya ya mazingira katika ngazi za cheti, stashahada na shahada ili kuhakiki utambuzi wa programu hizo, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuzuia changamoto kwa wahitimu watakaohitaji kusajiliwa na Baraza baada ya kumaliza masomo yao.










