
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo, tarehe 30 Oktoba 2026, amekutana na viongozi wa taasisi na makampuni mbalimbali ya Korea Kusini jijini Seoul, kujadili fursa za ufadhili, uwekezaji na upatikanaji wa utaalamu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo Zanzibar.

Katika mikutano hiyo iliyohusisha kampuni za K-FINCO, HEERIM, Sejong Plant, SAMOO C.M. Architects & Engineers na Sung Shin Rolling Stock Technology Ltd. (SSRST), majadiliano yamejikita katika miradi ya bandari, usafiri wa baharini, barabara, miundombinu ya mijini, nishati, utalii na viwanda, pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar (MICE).
Aidha, mazungumzo hayo yamehusu uwezekano wa ushirikiano katika miradi ya upatikanaji wa maji safi na salama, usafishaji wa maji taka, uwekezaji katika miundombinu ya kuhifadhi mazao ya uvuvi kwa njia ya baridi na upatikanaji wa masoko ya kimataifa.

Sambamba na hilo, kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology Ltd. imeonesha nia ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mpango wa kurejesha huduma za reli kwa ajili ya usafiri wa abiria na utalii Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mawasiliano ya kitaalamu kati ya pande hizo ili kuweka mikakati ya utekelezaji na kubainisha mifumo ya ufadhili wa miradi hiyo kwa kuzingatia taratibu za Serikali.









