Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linasikitishwa na vitendo vinavyoendelea vya uhujumu wa miundombinu ya umeme katika mikoa ya Iringa na Njombe, vinavyohusisha uchomaji wa nguzo za umeme na wizi wa transfoma.
Hadi sasa, jumla ya nguzo 66 zimeungua, huku moto ukiendelea kuwaka. Katika Mkoa wa Njombe, jumla ya nguzo 39 zimeungua katika maeneo ya Mgala (13), Utengule (3), Iboya (2), Image (2), Igoma (2), Utalingolo (4) na Yakobi (13). Katika Wilaya ya Makete, jumla ya nguzo 27 zimeungua katika maeneo ya Ikonda (16), Ilela (5), Ipelele (3) na Lupila (3).

Taarifa iliyotolewa na TANESCO Oktoba 28, 2026, imesema vitendo hivyo vimesababisha kukosekana kwa huduma ya umeme katika maeneo yanayoathirika na kuisababishia Shirika hasara, huku vikiathiri shughuli za kijamii na kiuchumi za wananchi.
“Katika Mkoa wa Njombe, nguzo zipatazo 66 zimeungua katika maeneo ya Yakobi, Iboya, Utalingolo, Image, Utengule, Igoma, Utalingolo, Makete, Ikonda, Ilela, Ipelele, Lupila na Mgala. Aidha, transfoma moja imeibiwa katika eneo la Mafinga, Wilaya ya Wanging’ombe,” imesema taarifa hiyo.
Kwa upande wa Mkoa wa Iringa, Wilaya ya Kilolo, nguzo 10 zimeungua, nyaya zimeharibika na transfoma moja yenye uwezo wa kVA 100 imeibiwa. Katika Wilaya ya Mafinga, nguzo tano zimeungua na transfoma mbili, kila moja yenye uwezo wa kVA 50, zimeibiwa.

TANESCO inakemea vikali vitendo hivyo na kuwaonya wote wanaohusika kuacha mara moja uharibifu na wizi wa miundombinu ya umeme.
Aidha, wananchi wanahimizwa kuchukua tahadhari wakati wa kuchoma moto kwa shughuli za kilimo na usafishaji wa mashamba ili kuzuia moto kusambaa na kuharibu miundombinu ya umeme.
Shirika linatoa wito kwa wananchi kushirikiana kulinda miundombinu hiyo kwa kutoa taarifa za wizi, uchomaji wa makusudi na uharibifu wa vifaa vya umeme kwa Jeshi la Polisi au kupitia namba ya huduma kwa wateja ya TANESCO, 180, ili hatua stahiki zichukuliwe.
Ulinzi wa miundombinu ya umeme ni wajibu wa kila mmoja wetu. Tushirikiane sote kukomesha vitendo vya hujuma na kuhakikisha huduma ya umeme inaendelea kuwa thabiti na endelevu.











