Home Kitaifa DIT YAHITIMISHA AWAMU YA PILI YA MAFUNZO YA KIDIGITALI, VIJANA 32 WANG’ARA

DIT YAHITIMISHA AWAMU YA PILI YA MAFUNZO YA KIDIGITALI, VIJANA 32 WANG’ARA

   Na Mwandishi Wetu.

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imehitimisha awamu ya pili ya mafunzo ya mradi wa majaribio unaolenga kuwawezesha vijana kutumia teknolojia ya kidigitali katika kujitangaza, kujiajiri na kuongeza fursa za ajira, huku vijana 32 waliokuwa wakishiriki mafunzo hayo wakihitimu.

Hafla ya kufunga mafunzo hayo imefanyika leo, Oktoba 02, 2026, katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia za kuwawezesha vijana kutumia ujuzi wa kidigitali katika kujiletea maendeleo na kuchangamkia fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidigitali.

Mafunzo hayo ya majaribio yamewalenga vijana kuwawezesha kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha ufanisi wa shughuli wanazofanya, ikiwemo shughuli za kibiashara, utengenezaji wa maudhui mtandaoni pamoja na kujitangaza kitaalamu kupitia majukwaa ya kidigitali.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Ezekiel Amri, amesema teknolojia ya habari ni moja ya nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa mtu binafsi, hususan vijana, pamoja na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Prof. Amri amewapongeza vijana hao kwa kukamilisha mafunzo hayo, akibainisha kuwa wote 32 walioanza mafunzo wameweza kuyamaliza, bila mshiriki hata mmoja kuacha njiani.

“Katika Dunia ya leo, suala la Teknolojia ya Habari ni mojawapo ya mambo yanayosaidia sana kukuza uchumi, kwa mtu binafsi hasa vijana kupitia shughuli mnazozifanya na pia uchumi wa Taifa. Napenda kuwapongeza sana, mmeanza mafunzo haya mkiwa 32 na mmeyamaliza mkiwa hao hao 32, hakuna aliyeishia njiani,” amesema Prof. Amri.

Aidha, Prof. Amri amewakaribisha vijana hao kuendelea kutumia fursa zinazopatikana DIT kwa ajili ya kuendeleza ujuzi walioupata, akieleza kuwa taasisi hiyo imejipambanua kwa kuwa na wataalamu waliobobea katika masuala ya teknolojia.

Amesema DIT ina wataalamu pamoja na vifaa vinavyoweza kuwawezesha vijana kupata mafunzo mbalimbali ya kiteknolojia, hivyo kuwataka wahitimu hao kutumia mafunzo waliyopata kama hatua ya kuendelea kujifunza kupitia kozi fupi zitakazotolewa na Kitengo cha ITCOEICT.

“Mafunzo haya yawafanye mfikirie kupata mafunzo zaidi ya kozi fupi mbalimbali zitakazotangazwa hapa na Kitengo chetu cha ITCOEICT. Hongereni sana na karibu sana DIT,” amesema Prof. Amri.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mafunzo, Kituo cha Umahiri wa TEHAMA – DIT, Bw. Othman Mfinanga, amesema mafunzo hayo yamekuja kutoa majibu kwa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili vijana katika kutumia teknolojia ya kidigitali kwenye shughuli zao.

Bw. Mfinanga amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa majaribio ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeuanzisha kwa kutambua umuhimu wa kuwawezesha vijana kutumia ujuzi wa kidigitali katika kuboresha shughuli zao.

Amesema kupitia mafunzo hayo, vijana wamepata nafasi ya kujifunza namna teknolojia inavyoweza kutumika katika kuongeza ufanisi wa shughuli mbalimbali, ikiwemo biashara na utengenezaji wa maudhui mtandaoni.

“Haya mafunzo ni mafunzo ya majaribio ambayo Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeona kwamba kuna haja ya kuwawezesha vijana katika shughuli zao ili waweze kutumia ujuzi wa kidigitali katika kuboresha ufanisi wa shughuli wanazozifanya, kama ni shughuli za kibiashara, utengenezaji wa maudhui mtandaoni na kadhalika,” amesema Bw. Mfinanga.

Naye mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Fredy Mwita, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Bahari, ameishukuru Serikali kwa kutoa fursa hiyo kwa vijana na kusema mafunzo hayo yatamsaidia kutumia maarifa aliyoyapata kwa namna yenye manufaa.

Fredy amesema anatarajia kutumia ujuzi huo katika shughuli zake na kuhakikisha maarifa aliyoyapata yanakuwa sehemu ya mchango wake chanya kwa maendeleo ya nchi.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa fursa muhimu kwa vijana kupata ujuzi unaoweza kuwasaidia katika mazingira ya sasa ambayo teknolojia ya kidigitali imekuwa sehemu muhimu ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa majaribio unaolenga kuwajengea vijana uwezo wa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano katika kuboresha shughuli zao, kujitangaza, kuongeza ufanisi, kukuza biashara na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia uchumi wa kidigitali.

IKUMBUKWE,  hii ni awamu ya pili ya mafunzo hayo kwa upande wa DIT. Awamu ya kwanza ilihitimishwa wiki iliyopita, ambapo vijana 48 walihitimu mafunzo hayo na kukabidhiwa vyeti vya utambuzi wa ushiriki wao. Leo, Oktoba 02, 2026, vijana wengine 32 wamehitimisha awamu ya pili, hivyo kuendelea kwa DIT katika kuwajengea vijana uwezo wa kutumia teknolojia ya kidigitali kama nyenzo ya kujiajiri, kujitangaza na kuongeza fursa za ajira.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!