Home Kitaifa WANANCHI MBULU KUNUFAIKA NA MITUNGI 3,255 YA GESI KWA BEI YA RUZUKU

WANANCHI MBULU KUNUFAIKA NA MITUNGI 3,255 YA GESI KWA BEI YA RUZUKU

Celebrating 25 Years of NHIF

📌 Nishati safi ya kupikia kwa kila Mtanzania

📍 Mbulu, Manyara

FAHARI AFYA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Ndugu Abubakar Kuuli kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo na wananchi, amepokea rasmi Mradi wa Usambazaji na Uuzaji wa Mitungi ya Gesi ya kilo sita kwa Bei ya Ruzuku, unaolenga kuongeza upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Mradi huo ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, ambao unalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa nishati zisizo safi na kulinda afya za wananchi pamoja na mazingira.

Mradi huo unatekelezwa na kusimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia kampuni ya Manjis Logistics Limited, ambayo imepewa jukumu la kusambaza na kuuza jumla ya mitungi 3,255 ya gesi kwa bei ya ruzuku katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mbulu.

Aidha, katika mradi huu mwananchi atanufaika kwa kupata mtungi mmoja wa gesi ulio kamili kwa matumizi, ukiwa na gesi pamoja na vifaa vyake vyote muhimu kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 17,500. Ili kupata huduma hiyo, mnunuzi anatakiwa kuwa na kitambulisho chake cha Taifa (NIDA).

Lengo kuu la mradi huo ni kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo ya vijijini kwa kuongeza upatikanaji wa majiko na mitungi ya gesi kwa gharama nafuu. Aidha, mradi unatarajiwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kudhibiti ukataji holela wa miti, kuhifadhi mazingira na kupunguza athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia.

Aidha, katika kuleta tija ya mradi wananchi wa Wilaya ya Mbulu wanahimizwa kutumia fursa hiyo kwa kujitokeza kununua mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!