Home Kitaifa KIHENZILE AHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA SEKTA YA UCHUKUZI NA MNYORORO WA...

KIHENZILE AHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA SEKTA YA UCHUKUZI NA MNYORORO WA UGAVI BARANI AFRIKA


Mgeni rasmi wa Mkutano wa 8 wa Afrika wa Uendeshaji na Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM 2026) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb.), akisisitiza matumizi ya teknolojia katika ufuatiliaji wa mizigo na kuwataka watafiti na wataalamu kutoa majawabu ya kiutendaji yatakayopunguza gharama za usafirishaji barani Afrika.


*****************

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, ameeleza kuwa mifumo bora ya usafirishaji ndiyo uti wa mgongo unaounganisha wazalishaji, masoko na fursa za kiuchumi barani Afrika.

Kihenzile amebainisha hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa 8 wa Afrika wa Uendeshaji na Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM) leo Septemba 22, 2026, katika Hoteli ya Mount Meru, Arusha.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Kihenzile amesema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya kimkakati ikiwemo reli, bandari, pamoja na usafiri wa anga na majini ili kuwezesha biashara na kukuza sekta ya utalii.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa miundombinu pekee haitoshi bila kuwepo kwa mabadiliko ya kidijitali na matumizi ya teknolojia mpya kama Akili Mnemba katika ufuatiliaji wa mizigo na ubadilishanaji wa taarifa.

Kwa upande wake, Mgeni Maalumu katika Mkutano huo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amebainisha kuwa lengo la mkutano huo ni kujenga ushirikiano thabiti na wa kimkakati unaounganisha vyuo vikuu na sekta ya viwanda katika nyanja za elimu, utafiti, na ubunifu.

Prof. Mwegoha amesema kuwa changamoto za kidunia kama mabadiliko ya tabianchi, msukosuko wa kiuchumi, na majanga ya afya zinaendelea kuathiri mifumo ya ugavi barani Afrika.

Alifafanua kuwa kujenga minyororo ya ugavi yenye ustahimilivu kunahitaji zaidi ya miundombinu na teknolojia kunahitaji bali rasilimali watu wenye ujuzi wa hali ya juu, tafiti za kuaminika, na taasisi zinazosimamia kwa madhubuti.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro, alisema mkutano wa mwaka huu imejikita katika mada za kimkakati kama matumizi ya Akili Mnemba (AI), mifumo endelevu ya ugavi katika huduma za afya, mfumo wa chakula na kilimo, pamoja na usafiri rafiki kwa mazingira.

Prof. Hawa alitoa wito kwa vyuo vikuu kutathmini mara kwa mara mitaala na mbinu za ufundishaji ili kuandaa wahitimu wenye umahiri wa kidijitali, fikra changanuzi, na uongozi wenye maadili unaoendana na mabadiliko ya haraka ya soko la ajira.

Matokeo na mapendekezo yatakayopatikana katika siku hizi mbili yanatarajiwa kutoa dira mpya katika mnyororo wa ugavi kama njia pekee ya kuijenga Afrika yenye ustahimilivu wa kiuchumi na kugeuza tafiti za kitaaluma kuwa suluhisho kwa sekta husika.

Mgeni Maalumu wa Mkutano wa 8 wa Afrika wa Uendeshaji na Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM 2026) ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha akibainisha kuwa mkutano huo ni matokeo ya ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuimarisha elimu, utafiti, na mahusiano kati ya vyuo vikuu na sekta ya uchukuzi.



Mgeni rasmi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb.), akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe, wawakilishi wa Kühne Foundation na Learn Logistics, pamoja na washiriki wa Mkutano wa 8 wa Afrika wa Uendeshaji na Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM 2026) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo leo tarehe 22 Septemba 2026, katika Hoteli ya Mount Meru-Arusha.







Washiriki wa Mkutano wa 8 wa Afrika wa Uendeshaji na Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM 2026) wakifuatilia mada na mijadala mbalimbali inayowasilishwa wakati wa ufunguzi wa mkutano huo leo tarehe 22 Septemba 2026 katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe – Taaluma, Utafiti na Ushauri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano wa 8 wa Afrika wa Uendeshaji na Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM 2026), Prof. Hawa Tundui Petro, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha tafiti za kitaaluma na changamoto halisi za jamii na sekta ya uchukuzi, huku akihimiza uboreshaji wa mitaala ili kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi wa kidijitali, ubunifu, na fikra changanuzi kulingana na soko la sasa la ajira.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!