Home Afya TANZANIA HAINA MGONJWA WA EBOLA, ULINZI WA AFYA WAIMARISHWA

TANZANIA HAINA MGONJWA WA EBOLA, ULINZI WA AFYA WAIMARISHWA

Tanzania inaendelea kuwa salama dhidi ya ugonjwa wa Ebola, huku Serikali ikisisitiza kuwa hakuna mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na maambukizi hayo nchini. Mamlaka za afya zimeendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi na ufuatiliaji ili kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini kutokana na mlipuko unaoendelea katika baadhi ya nchi jirani, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda.

Akizungumza na umma kuhusu hali ya tishio la Ebola na hatua za kuimarisha utayari wa taifa Juni 18, 2026, jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha ugonjwa huo haupenyi nchini kupitia mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji, utambuzi wa mapema na udhibiti wa magonjwa.

Amesema tangu kutangazwa kwa mlipuko huo mwezi Mei mwaka huu, hatua mbalimbali za kinga zimeendelea kutekelezwa, ikiwemo utoaji wa Mwongozo wa Wasafiri (Travel Advisory) Na. 17 wa Mei 19, 2026, unaotoa maelekezo na tahadhari kwa wasafiri wote wanaoingia nchini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, ufuatiliaji wa taarifa na tetesi zinazohusiana na Ebola umeimarishwa katika jamii na maeneo ya mipakani. Hadi sasa, jumla ya tetesi 64 kutoka mikoa 21 zimeripotiwa, ambapo wahisiwa 11 walifanyiwa uchunguzi na vipimo vilivyothibitisha kuwa hawakuwa na maambukizi ya Ebola.

“Mpaka sasa nchi yetu haina mgonjwa wa Ebola na hali ya usalama wa afya nchini inaendelea kuwa nzuri. Hata hivyo, tunaendelea kuchukua hatua zote muhimu za tahadhari ili kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini,” amesema Mchengerwa.

Aidha, amesema uwezo wa vituo vya kutolea huduma za afya na wataalamu umeongezwa kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vifaa vya kujikinga kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo endapo utatokea.

Pia, Serikali imehakikisha uwepo wa akiba ya kutosha ya vifaa maalumu vya kujikinga kupitia Bohari ya Dawa (MSD) na katika mikoa yote nchini kwa matumizi ya dharura, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa wahudumu wa afya waliopo mstari wa mbele.

Katika kuimarisha uwezo wa uchunguzi na utambuzi wa ugonjwa huo, maabara mbili jongezi zimeanzishwa katika mikoa ya Kagera na Kigoma ili kurahisisha upimaji wa sampuli karibu na maeneo yanayopakana na nchi zilizoathirika.

Mchengerwa amesema zaidi ya watoa huduma za afya 45,000 wamepatiwa mafunzo ya ana kwa ana na kwa njia ya mtandao kuhusu kinga, utambuzi na udhibiti wa Ebola. Vilevile, elimu ya afya inaendelea kutolewa kwa wananchi, wasafiri na wakazi wa maeneo ya mipakani ili kuongeza uelewa na kuimarisha tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!