Home Kitaifa RUZUKU YA SERIKALI YAPUNGUZA GHARAMA ZA MBOLEA KWA WAKULIMA

RUZUKU YA SERIKALI YAPUNGUZA GHARAMA ZA MBOLEA KWA WAKULIMA

Serikali kupitia Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) imewahakikishia wakulima nchini upatikanaji wa mbolea ya kutosha kwa msimu wa kilimo wa mwaka huu, ikitangaza kuanza kwa usambazaji wa tani 33,000 za mbolea ya kupandia aina ya DAP zilizowasili nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza leo Agosti 4,2026 katika Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea kitaifa katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uendeshaji Biashara wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Lameck Borega, amesema kampuni hiyo imejipanga kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa wakati, kwa bei nafuu na katika maeneo yote ya nchi.

Amesema TFC, ambayo ni kampuni inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali chini ya Wizara ya Kilimo, ina jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakulima wote ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Bw.Borega amesema kwa msimu wa mwaka huu kampuni imepanga kusambaza takribani tani 200,000 za mbolea za aina mbalimbali, huku meli ya MV Aurora ikiwa tayari imewasili na tani 33,000 za mbolea ya DAP ambazo zimeanza kusafirishwa kwenda vituo vya TFC na kwa mawakala wake nchini kote.

“Mbolea hii imewasili kwa wakati muafaka wakati wakulima wengi wanaendelea kuandaa mashamba yao kwa ajili ya msimu mpya wa kilimo. Lengo letu ni kuhakikisha hakuna mkulima anayekosa mbolea kutokana na ucheleweshaji wa usambazaji,” amesema Borega.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kubeba sehemu kubwa ya gharama za mbolea kupitia mpango wa ruzuku ili kupunguza mzigo kwa wakulima. Alifafanua kuwa mfuko mmoja wa kilo 50 wa mbolea ya DAP ungegharimu karibu shilingi 200,000 bila ruzuku, lakini kutokana na msaada wa Serikali mkulima analipa karibu nusu ya gharama hiyo huku Serikali ikigharamia sehemu iliyobaki.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwa kuhakikisha pembejeo muhimu zinapatikana kwa gharama zinazomuduwa na wakulima.

Bw.Borega ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa usambazaji wa mbolea ya kupandia, Serikali inatarajia kuingiza nchini tani 40,000 za mbolea ya kukuzia aina ya Urea mwezi Septemba, hatua itakayowezesha wakulima kupata pembejeo zote muhimu katika kipindi sahihi cha uzalishaji.

“Niwaondoe wasiwasi wakulima wote nchini Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha mbolea inapatikana kwa wakati na kwa mfumo wa ruzuku ili kila mkulima aweze kunufaika na kuongeza uzalishaji wa mazao,” amesema 

Sambamba na hilo,Bw. Borega amewataka wakulima wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kutembelea  banda la TFC ili kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, namna ya kunufaika na mfumo wa ruzuku na mahali pa kupata mbolea hizo.

Amesema TFC pia inaendelea kushiriki maonesho ya Nanenane katika kanda mbalimbali nchini ikiwemo Mbeya, Arusha, Mwanza, Simiyu, Iringa na Morogoro, ambako wakulima wanaendelea kupewa elimu ya kitaalamu kuhusu matumizi bora ya mbolea na njia rahisi za kuzipata kupitia mtandao wa vituo na mawakala wa kampuni hiyo.

Hata hivyo amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya mbolea ni nguzo muhimu ya kuongeza tija ya kilimo, hivyo akawataka wakulima kutumia fursa ya maonesho hayo kupata elimu itakayowawezesha kuongeza uzalishaji na kuinua kipato chao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!