Naibu Katibu Mkuu Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu,Prof Daniel Mushi,akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa TESP na kuhitimisha mradi huo uliofanyika leo Aprili 9,2026 jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI imesisitiza umuhimu wa kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia Mradi wa Kusaidia Elimu ya Ualimu (TESP), ili kuhakikisha ubora wa elimu unaimarika kwa vizazi vijavyo.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu,Prof Daniel Mushi, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa TESP na kuhitimisha mradi huo uliofanyika leo Aprili 9,2026 jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo.
Amesema kikao hicho si tu hitimisho la mradi, bali ni fursa ya kufanya tathmini, kujifunza na kuweka mikakati ya kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaendelea kudumishwa na kupanuliwa.
Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Prof. Mushi ameishukuru Serikali ya Canada kupitia taasisi ya Global Affairs Canada kwa ushirikiano na msaada wao uliochangia kuimarisha mifumo ya elimu ya ualimu nchini.
Ameeleza kuwa tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2017, kumekuwa na maboresho makubwa ikiwemo usambazaji wa zaidi ya vitabu laki moja tisini na sita katika vyuo 35 vya ualimu pamoja na kuunganishwa kwa taasisi hizo na mtandao wa maktaba za vyuo vikuu nchini.
Aidha, zaidi ya vifaa 1,400 vya TEHAMA vimesambazwa, hatua iliyosaidia kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, huku miundombinu kama maktaba na maabara ikijengwa na kukarabatiwa.
Katika hatua nyingine, zaidi ya wakufunzi 1,300 wamepatiwa mafunzo ya mbinu za kisasa za ufundishaji, elimu jumuishi pamoja na matumizi ya teknolojia, huku takribani walimu wanafunzi 73,000 wakihitimu katika kipindi cha mradi huo.
Prof. Mushi amesema mafanikio hayo ni uwekezaji mkubwa katika mustakabali wa elimu nchini, lakini akasisitiza kuwa ni muhimu sasa kuhakikisha yanaendelezwa kupitia ufadhili endelevu, uongozi imara wa taasisi na matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo.
Ametoa wito kwa washiriki wa kikao hicho kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza miradi hiyo, kupanua mafanikio yake katika taasisi nyingine na kuimarisha ushirikiano kati ya wizara, taasisi na wadau wa maendeleo.
Ametangaza rasmi kufunguliwa kwa kikao hicho huku akisisitiza kuwa jukumu lililopo sasa ni kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelea kuleta matokeo chanya kwa muda mrefu.


























