Home Kitaifa NYUMBA 560 ZAUZWA, NHC YANG’ARA KATIKA SEKTA YA MAKAZI

NYUMBA 560 ZAUZWA, NHC YANG’ARA KATIKA SEKTA YA MAKAZI

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeandika historia mpya katika sekta ya makazi baada ya kuuza nyumba zote 560 za Mradi wa Samia Housing Scheme uliopo Kawe kabla hata ya kukamilika kwa ujenzi wake, hatua inayoakisi mafanikio makubwa ya mradi huo.

Mafanikio hayo yalibainishwa Machi 25, 2026 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Serikali (PIC), ambapo Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alisema mauzo hayo yamepunguza utegemezi wa mikopo ya benki licha ya mpango wa awali wa kukopa Sh30 bilioni.

Abdallah alieleza kuwa hatua hiyo imeongeza uwezo wa NHC kujitegemea kifedha huku ikiendesha miradi yake kwa ufanisi zaidi. Aliongeza kuwa baadhi ya wanunuzi tayari wamehamia kwenye nyumba hizo, huku wengine wakizitumia kama vitega uchumi kupitia upangishaji.

Mradi huo una thamani ya Sh49 bilioni, ambapo zaidi ya Sh45 bilioni tayari zimetumika, jambo linaloonesha kasi ya utekelezaji wake.

Katika kuimarisha maendeleo jumuishi, NHC imeweka miundombinu ya kijamii ndani ya mradi huo, ikiwemo shule za kisasa na uwanja wa michezo wenye uwezo wa kuhudumia takribani watu 15,000 kwa lengo la kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo.

Aidha, shirika hilo linatarajia kuyakarabati majengo ya zamani ya iliyokuwa Tanganyika Packers na kuyageuza kuwa masoko ya kisasa (bazaar) yatakayochochea shughuli za kiuchumi na kutoa huduma za bidhaa za kila siku.

Kwa upande wa ujenzi, Mhandisi wa mradi huo, Grace Msita, alisema mradi unahusisha majengo 10 (Block A hadi J) yenye aina tatu za nyumba.

Nyumba hizo ni pamoja na 240 za vyumba vitatu (sqm 89) zilizouzwa kwa Sh192.7 milioni kila moja, 160 za vyumba viwili (sqm 68) kwa Sh147 milioni kila moja, na 160 za chumba kimoja (sqm 21.2) kwa Sh38.8 milioni kila moja.

Aliongeza kuwa NHC ilisimamia ujenzi kama mkandarasi mkuu, huku vifaa vingi vikitengenezwa ndani ya shirika na kuthibitishwa na taasisi kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Mbali na mafanikio ya kifedha, mradi huo umechangia ajira kwa zaidi ya watu 1,800 wakiwemo mafundi na watoa huduma mbalimbali. Aidha, zaidi ya wanafunzi 630 walipata mafunzo ya vitendo, huku wahitimu 47 wakiajiriwa moja kwa moja na wengine zaidi ya 100 wasiokuwa na taaluma rasmi wakipata kipato.

Wajumbe wa Kamati ya PIC walieleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo, wakipongeza ubunifu na usimamizi mzuri wa uwekezaji wa umma.

Hata hivyo, ziara hiyo ilisimamishwa baada ya kupokelewa taarifa ya kifo cha mbunge mwenzao, William Lukuvi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!