WATUMISHI wa Tume ya Ushindani Ofisi ya Kanda ya Ziwa wametoa elimu kwa wadau mbalimbali, wakiwemo wanafunzi, waandishi wa habari na wafanyabiashara, walipotembelea Banda la Kliniki ya Walaji katika Manispaa ya Musoma Mkoani Mara.
Banda hilo limegeuka kuwa kitovu cha maarifa, likiwavutia wengi waliotaka kuelewa kwa undani haki zao kama walaji pamoja na namna bora ya kushiriki katika soko kwa uadilifu na uelewa mpana.
Akitoa elimu hiyo, Mkuu wa Kanda ya Ziwa FCC, Bw. Mdimi, amesisitiza umuhimu wa walaji kuwa na uelewa wa haki zao ili kujilinda dhidi ya bidhaa duni, huduma zisizo na viwango na vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kujitokeza sokoni.
“Amebainisha kuwa elimu kwa walaji ni silaha muhimu katika kujenga uchumi imara unaozingatia haki na usawa kwa wote.”amesema Bw.Mdimi
Kwa upande wa wafanyabiashara, wamekumbushwa umuhimu wa kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria za ushindani wa haki, wakielezwa kuwa uaminifu kwa wateja ni msingi wa mafanikio ya biashara yoyote endelevu.
Elimu hiyo imewajengea uelewa mpya kuhusu wajibu wao katika kulinda maslahi ya walaji.
Wanafunzi wameahidi kuwa mabalozi wa elimu hiyo katika jamii zao, huku waandishi wa habari wakiahidi kueneza ujumbe huo kwa umma kupitia vyombo vyao.
Elimu hiyo ni sehemu ya maandalizi kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Siku ya Haki za Mlaji Duniani 2026, yakilenga kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda haki za walaji na kuimarisha ushindani wa haki sokoni.
Kwa ujumla, juhudi hizi zinaakisi dhamira ya Tume ya Ushindani kuhakikisha kuwa kila mlaji anakuwa na sauti, analindwa na anapata huduma bora, huku biashara zikikua katika mazingira ya haki na uwazi.


















