Home Kitaifa PIC YAAHIRISHA ZIARA BAADA YA KIFO CHA LUKUVI

PIC YAAHIRISHA ZIARA BAADA YA KIFO CHA LUKUVI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeahirisha ziara yake katika miradi ya Samia Housing na 711 Kawe inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Mwenyekiti wa PIC, Masanja Kadogosa amewatangazia wajumbe wa kamati hiyo akieleza ni kufuatia kifo cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Wenye Ulemavu), William Lukuvi, kilichotokea leo Machi 25,2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma.

Kadogosa amefafanua kuwa wameahirisha ziara hiyo kwa mujibu wa taratibu za kibunge ili kupisha taratibu za msiba. Amesema Bunge limepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mbunge mwenzao.

Kadogosa ametoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote, akieleza kuwa Lukuvi alikuwa kiongozi muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya serikali, hasa katika masuala ya sera.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, amesema shirika limepokea kwa masikitiko taarifa hiyo na kutoa pole kwa Rais na Spika wa Bunge. Ameongeza kuwa Lukuvi aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na alisimamia kuanza kwa mradi wa 711 Kawe, hivyo NHC imepoteza kiongozi mwenye maono makubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!