Home Kitaifa EWURA KUHAKIKISHA UPATIKANAJI WA MAFUTA KWA WAKATI

EWURA KUHAKIKISHA UPATIKANAJI WA MAFUTA KWA WAKATI

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeagizwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli nchini unaendelea bila vikwazo, huku ikikataza wafanyabiashara kuhifadhi mafuta kwenye maghala kwa lengo la kusubiri kupanda kwa bei.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati, Mh. Deogratius Ndejembi, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zinazohusika na mafuta nchini, zikiwemo EWURA, Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Kikao hicho kilifanyika katika ofisi za EWURA, Machi 23, 2026.

Akizungumza katika kikao hicho, Mh. Ndejembi aliagiza EWURA kufanya ukaguzi wa maghala yote ya mafuta nchini ili kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hizo unaanzia Bandari ya Dar es Salaam hadi maeneo ya mipakani, ikiwemo Kyerwa, bila kuwepo kwa upungufu.

Aidha, Mh. Ndejembi alisema kuwa nchi ipo salama kwa upande wa upatikanaji wa mafuta na kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo bila vikwazo. Alisisitiza kuundwa kwa timu maalum itakayojumuisha EWURA, PBPA na TPDC kwa ajili ya kufuatilia uingizaji wa mafuta nchini, ili kuhakikisha mafuta yote yaliyoagizwa yanawasili kwa wakati.

“Timu hii itahakikisha mafuta yote yaliyoagizwa yanawasili bila kikwazo, kwani hali ya biashara ya mafuta duniani si ya kuridhisha,” alisema Mhe. Ndejembi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, James Mataragio, alisema kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta hadi Julai 2026, huku Wizara ikiendelea kusimamia usafirishaji wa mafuta ili kudhibiti vitendo vya upandishaji bei kiholela.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Mwainyekule, alisema EWIRA itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maghala ya kuhifadhia mafuta pamoja na kushirikiana na wadau wa sekta hiyo, wakiwemo wasambazaji wa mafuta, ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, alisema Serikali imehakikisha upatikanaji wa mafuta ya kutosha kupitia mikataba ya uingizaji wa mafuta iliyofanyika mapema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!