
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), amesema Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Austria ili kuhakikisha malengo ya Mkakati mpya wa Austria–Africa wa mwaka 2026 hadi 2029 yanafikiwa kama yalivyopangwa.
Mhe. Munde aliyasema hayo alipokutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Mhe. Hannah Liko, katika kikao kilichojadili mkakati wa Austria wa kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika, ikiwemo ushirikiano wa kukuza uchumi kati ya Austria na Tanzania. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Alisema mkakati huo mpya wa Austria–Africa wa mwaka 2026 hadi 2029 umejikita katika maeneo makuu manne ambayo ni amani na usalama, ushirikiano wa kiuchumi, uhamiaji, pamoja na elimu na sayansi.
“Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, iko tayari kushirikiana na Austria kutekeleza mkakati huo kwa maendeleo ya watu wa pande zote mbili, na inatarajia kuona ushirikiano ukikua zaidi katika sekta za umma na binafsi,” alieleza Mhe. Munde.

Alifafanua kuwa katika nyanja ya amani, pande zote mbili zinalenga kuimarisha uthabiti kupitia ushirikiano na Umoja wa Mataifa katika kuzuia migogoro. Kwa upande wa uchumi, mkakati unalenga kukuza uwekezaji na fursa za uchumi wa kijani ili kutengeneza ajira na kuboresha miundombinu.
Aidha, aliongeza kuwa mkakati huo utashughulikia suala la uhamiaji kwa kupambana na biashara haramu ya binadamu na kukuza uhamiaji wa kisheria wenye tija. Katika sekta ya elimu, kutaanzishwa vituo vya umahiri pamoja na programu za ufadhili wa masomo katika nyanja za maji, nishati, afya na mifumo ya kidijitali.
Aliongeza kuwa mkakati huo unatazamwa kama daraja muhimu kuelekea Dira ya Tanzania 2050, ukisisitiza ushirikiano wa usawa na wenye faida kwa pande zote mbili. Pia aliitaka sekta binafsi ya Austria kutumia fursa zilizopo nchini, ikiwemo katika sekta za kilimo, nishati na mazingira, ili kuwekeza zaidi.
Vilevile, Mhe. Munde aliishukuru Austria kwa msaada wake unaoendana na vipaumbele vya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (FYDP III) pamoja na Dira ya Maendeleo ya 2025, wakati nchi ikijiandaa kuanza rasmi utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 iliyozinduliwa hivi karibuni.
Alibainisha kuwa Austria inafadhili miradi mikubwa ya kimkakati nchini yenye thamani ya Euro milioni 30 kupitia mikopo nafuu. Miradi hiyo ni pamoja na ukarabati na uboreshaji wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) Zanzibar (Euro milioni 7), uboreshaji wa mfumo wa elimu Zanzibar (Euro milioni 6), ununuzi wa magari ya zimamoto na vifaa vya uokoaji Zanzibar (Euro milioni 10), pamoja na ukarabati wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) uliogharimu Euro milioni 7.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria, Mhe. Hannah Liko, aliipongeza Tanzania kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kukuza uchumi, akieleza kuwa amani imechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia wawekezaji kutoka nje. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutumia fursa hiyo kujitangaza zaidi ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Aliongeza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania, katika kuhakikisha sekta binafsi inashirikishwa kikamilifu katika fursa za kiuchumi ili kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, alisema Austria ina kampuni zinazofanya kazi nchini, ikiwemo Andritz, ambayo imechangia katika miradi ya umeme wa maji, kahawa na korosho. Alieleza kuwa uwepo wa kampuni za Austria nchini umechangiwa kwa kiasi kikubwa na amani iliyopo, hivyo kuna uwezekano wa kuongeza uwekezaji zaidi siku zijazo.








