
Watumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zinazosimamia sekta hiyo wametakiwa kuhakikisha wanakuwa chachu ya maendeleo ya biashara badala ya kuwa vikwazo, ili kuchochea uzalishaji mkubwa wa bidhaa na kukuza uchumi wa viwanda nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara yake katika Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi kufanya kazi kwa weledi, kujituma na kubadilika kulingana na mahitaji ya sasa ya maendeleo ya viwanda ambayo yanahimizwa na Rais Samia Suluhu Hassan, huku akihimiza pia ushirikiano wa pamoja ili biashara zikue na viwanda viongezeke nchini.
“Tusimame pamoja, tufanye kazi, biashara ifanyike, viwanda vijengwe vya kutosha,” amesema.

Aidha, amesema wizara inapaswa kuondoka kwenye mtazamo wa udhibiti pekee na kuelekea katika kuwezesha biashara ili wananchi wanufaike na fursa za kiuchumi na kuzalisha mabilionea wazalendo.
“Serikali kama hatuwezi kuwapa mtaji, tutengeneze mazingira ya unafuu kwa wabunifu,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi, ikiwemo kuhakikisha wananchi wanafahamu shughuli zinazofanywa na shirika hilo kupitia vijana wabunifu.








