Home Kitaifa CG MWENDA AONYA WANAODANGANYA KUFUTA MADENI YA KODI

CG MWENDA AONYA WANAODANGANYA KUFUTA MADENI YA KODI

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda amewataka wafanyabiashara wenye madeni ya kodi kufika kwenye ofisi za mamlaka hiyo kutafuta suluhu badala ya kuhangaika na madalali mitaani ambao hawana uwezo wa kuwasaidia kufuta madeni hayo.

Akizindua kituo cha huduma za Kodi cha Masaki jijini Dar es Salaam kinachohudumiwa na mkoa wa Kodi Kinondoni February 17, 2026 Kamishna Mkuu Mwenda amesema kuna madalali wamekuwa wakiwadanganya wafanyabiashara kuwa wanauwezo wa kuwafutia madeni yao jambo ambalo haliwezekani.

Amesema kwa kawaida deni la kodi halifutiki mpaka mhusika anapoamua kulilipa au kulipinga na kushinda kesi mahakamani.

Kwa mujibu wa sheria za kodi hakuna mwenye mamlaka ya kufuta au kupunguza deni la kodi, kinachoweza kufuta au kuondoa deni la kodi ni kulilipa deni hilo na siyo vinginevyo, hivyo wanaowadanganya kuwa watawafutia madeni ya kodi wanawapotezea muda wenu lakini madeni yanabaki palepale” amesema Mwenda.

Amebainisha kuwa kinachotokea kwa wanaokaa na madeni hayo muda mrefu ni kukutana na riba pamoja na adhabu ambazo watapaswa kuzilipa hivyo wanapaswa kufuata utaratibu.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mwenyekiti wa chama cha washauri wa kodi Bi. Victoria Soka amewataka walipakodi kushirikiana na washauri wa kodi waliosajiliwa katika kutatua changamoto zao za kodi badala ya kudanganywa na madalali wa kodi ambao hawana utalaam wowote.

Amesema wapo washauri wengi wa kodi waliosajiliwa kwa nchi nzima ambao wamekuwa wakitoa huduma ili kuhakikisha walipakodi hawakutani na changamoto na wanalipa kodi kwa hiari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!