Na Job Karongo
HALMASHAURI ya Mji Handeni imeendelea kuonyesha mafanikio katika utekelezaji wa mpango wa lishe shuleni baada ya jumla ya wanafunzi 28,047 kati ya 30,898, sawa na asilimia 91, wanaosoma shule za msingi na sekondari kuendelea kupata chakula wakiwa shule.
Taarifa hiyo imetolewa na Afisa Lishe wa Halmashauri ya Mji Handeni, Esther Herman, wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa Robo ya Pili ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za lishe kilichohudhuriwa na viongozi wa halmashauri pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Amesema kuwa mpango huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha afya za wanafunzi, kuongeza mahudhurio shuleni pamoja na kuinua kiwango cha ufaulu kutokana na wanafunzi kuwa na umakini zaidi darasani.
Amebainisha kuwa utoaji wa chakula shuleni ni sehemu ya mkakati wa halmashauri wa kuboresha lishe kwa watoto wa umri wa shule, huku ukilenga pia kupunguza tatizo la utoro na kuongeza motisha ya wanafunzi katika masomo.
Kwa mujibu wa Afisa Lishe huyo, mafanikio ya mpango huo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya halmashauri, uongozi wa shule, wazazi na wadau wa maendeleo ambao kwa pamoja wamekuwa wakichangia upatikanaji wa chakula shuleni.
Hata hivyo, ametoa wito kwa shule na jamii kwa ujumla kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha wanafunzi wote waliosalia wanafikiwa na huduma ya chakula shuleni, kwa lengo la kufikia asilimia 100 ya wanafunzi wote katika halmashauri hiyo.












