Home Kitaifa SERIKALI YASISITIZA UTOAJI HUDUMA BORA UTEKELEZAJI BIMA YA AFYA

SERIKALI YASISITIZA UTOAJI HUDUMA BORA UTEKELEZAJI BIMA YA AFYA

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohammed Mchengerwa, amewataka viongozi na watendaji wa sekta ya afya nchini kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ya mwaka 2023 unakwenda sambamba na utoaji wa huduma bora, zenye utu na zisizo na ubaguzi kwa mwananchi.

Dkt. Samizi ameyasema hayo Desemba 19, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha viongozi wa sekta ya afya kilicholenga kutoa taarifa ya hatua iliyofikiwa kwenye maandalizi ya utekelezaji wa sheria hiyo, akibainisha kuwa maandalizi muhimu yamekamilika kabla ya kuanza usajili rasmi wa wananchi ndani ya mfumo wa bima ya afya kwa wote.

Amesema utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya kutafsiri maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha huduma za afya zinamfuata mwananchi badala ya mwananchi kuzifuata huduma, sambamba na kauli mbiu ya “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.”

Akizungumzia kuhusu maandalizi ya Serikali, Dkt. Samizi amesema Serikali imeendelea kuimarisha mazingira wezeshi ya utoaji huduma kwa kuongeza ajira za watumishi wa afya, kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya, kuboresha upatikanaji wa dawa pamoja na kununua na kusimikwa kwa vifaa tiba na vifaa vya kisasa.

“Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inaweka msisitizo wa kila mwananchi kuwa na bima ya afya itakayomuwezesha kumudu gharama za matibabu na kupata huduma kwa uhakika pindi anapozihitaji,” amefafanua Dkt. Samizi

Dkt. Samizi amevutaka vituo vya kutolea huduma za afya kuimarisha madawati ya huduma kwa wateja na mifumo ya utoaji wa mrejesho, pamoja na kupitia maoni ya wananchi kwa vikao vya kiutawala ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuendeleza yale yanayofanya vizuri.

Dkt. Samizi pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia utaratibu wa rufaa kwenye utoaji wa huduma za afya, akizitaka hospitali za rufaa za mikoa, kanda, Maalum na Taifa kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma katika ngazi stahiki kwa manufaa ya wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!