
Watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wamehimizwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kutumia maarifa yao ipasavyo ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, Jijini Dodoma Desemba 15, 2025 wakati wa kikao kazi na watumishi wa Wakala, akisema kuwa licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka mitano, bado kuna wajibu mkubwa wa kuendelea kufanya kazi kwa juhudi zaidi kwa kuwa wananchi wa vijijini wanategemea REA katika upatikanaji wa nishati.

Alieleza kuwa kila Idara na Kitengo ndani ya Wakala kina jukumu la kutekeleza majukumu yake kikamilifu ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuwapatia wananchi nishati bora, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja bila kuangalia tofauti za kiutendaji.
Aidha, aliwahimiza watumishi kudumisha mshikamano, kuheshimiana, kupendana na kuepuka migogoro pamoja na majungu katika maeneo ya kazi, huku akiwashauri kushughulikia changamoto kwa njia ya mawasiliano na kufuata taratibu sahihi ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Mhandisi Saidy alibainisha kuwa umeme ni kichocheo muhimu cha maendeleo na si anasa, na kwamba wananchi waishio vijijini wana matarajio makubwa ya kuunganishiwa huduma hiyo. Aliongeza kuwa vijiji vyote nchini tayari vimefikishiwa umeme, huku zoezi la kusambaza umeme vitongojini likiendelea kwa kasi kubwa.
Alifafanua kuwa hadi sasa vitongoji 17,500 tayari vimepata au vimeingizwa katika miradi na mipango ya kupatiwa umeme, na kubaki vitongoji 13,500 pekee. Alisisitiza kuwa REA ina wajibu wa kuhakikisha vitongoji vilivyobaki navyo vinaunganishwa na huduma ya umeme kabla ya mwaka 2030.
Vilevile, aliwahamasisha watumishi kujenga tabia ya kufanya mazoezi ya mwili kwa ajili ya kuimarisha afya na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi zao za kila siku.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa REA, Renatus Msangira, aliwakumbusha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili kudumisha maadili na uwajibikaji kazini.








