


Na: Secilia Edwin
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hifadhi Ameir, amemtaka mkandarasi wa COMFIX & Engineering kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa Kujenga Ujuzi na Ushirikiano Afrika Mashariki (EASTRIP) unaotekelezwa katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Kampasi ya Mwanza, ili ukamilike kwa wakati uliopangwa.

Akizungumza leo, Desemba 14, 2025, jijini Mwanza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Wanu amesema ucheleweshaji wa utekelezaji unaweza kuathiri malengo ya Serikali ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi kwa wakati unaohitajika katika soko la ajira la kimataifa, kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Wanu amesema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya kimkakati ya elimu ya ufundi na teknolojia, hivyo hakuna sababu ya mradi huo kuchelewa kukamilika. Amewataka wazabuni kuhakikisha vifaa vinawasili na kufungwa kwa wakati ili mafunzo yaanze kama ilivyopangwa.

Pia amebainisha kuwa Serikali imepanga kuongeza uwezo wa Kampasi ya DIT Mwanza kwa kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 300 hadi 2,000, hatua inayolenga kuongeza idadi ya vijana wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema kupitia Mradi wa EASTRIP, Kampasi ya DIT Mwanza inajenga kituo cha kikanda cha umahiri katika uchakataji na utengenezaji wa bidhaa za ngozi.
Profesa Mushi ameongeza kuwa kituo hicho kinajumuisha majengo matano yanayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 37, huku utekelezaji wa mradi huo ukiwa ni ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Dunia.
Naye Mkurugenzi wa Kampasi ya DIT Mwanza, Dk. John Msumba, amesema mradi wa EASTRIP umechangia kufufua sekta ya ngozi nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa wataalamu wa ndani na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.








