
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Issa Ndemanga, ametoa wito kwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali, sambamba na kushirikiana na wataalamu wa Halmashauri ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza leo Desemba 6, 2025, katika mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika Ukumbi wa Canteen, uliopo katika Ofisi za Halmashauri ya Chalinze, Mhe. Ndemanga amesema kuwa Halmashauri ina jukumu kubwa la kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unaendelea kufanyika kwa ufanisi kama ilivyoelekezwa na Serikali.

Aidha, Mhe. Ndemanga alibainisha kuwa katika kipindi ambacho madiwani hawakuwepo baada ya kumalizika kwa mchakato wa uchaguzi, watendaji waliendelea kutekeleza majukumu yao, na sasa anatarajia Halmashauri hiyo kuendeleza utendaji mzuri kwa ushirikiano wa madiwani waliorejea kazini.
Pia, Mhe. Ndemanga alisisitiza umuhimu wa umoja miongoni mwa madiwani na wananchi waliowachagua, huku akisema kuwa maendeleo ya Chalinze yatapatikana endapo kutakuwa na mshikamano na uongozi unaofanya kazi kwa pamoja.

Sambamba na hilo, aliwataka madiwani kuepuka migogoro na wataalamu wa Halmashauri, akisisitiza kuwa mgongano kati ya watoa maamuzi na wataalamu unasababisha ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo.
Kadhalika, aliwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika mabaraza ya madiwani na kufuatilia mijadala inayoendelea, akibainisha kuwa mikutano hiyo ni muhimu kwa uwazi na uwajibikaji.
“Wananchi mnaalikwa kuhudhuria mabaraza haya ili msikie madiwani wenu wanajadili nini kwa ajili ya maendeleo. Ukiona jambo ambalo hukulielewa, una nafasi ya kuwasilisha hoja yako kwa Katibu wa Baraza kwa mujibu wa kanuni,” alisema Mhe. Ndemanga.
Mhe. Ndemanga alihitimisha kwa kusisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika mabaraza ni nyenzo muhimu ya kuwapa mrejesho viongozi wao na kuchochea uwazi katika kusimamia maendeleo ya Wilaya ya Chalinze.








