
Mkuu wa wilaya ya Hanang Mheshimiwa Almishi Hazali ametoa wito kwa wananchi wa wilaya ya Hanang kujitokeza kwa wingi kununua majiko banifu ambayo yameanza kusambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku ya Tsh 11,200. Wito huo umetolewa tarehe 20 Novemba, 2025 alipofika Tarafa ya Katesh Kata ya Nangwa kijiji cha Nangwa kukagua na kufuatilia utekelezaji wa mradi wa majiko 1,583 yatakayosambazwa wilaya nzima.

Amesema kuwa mradi huu unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni mwendelezo wa juhudi za serikali katika kutunza mazingira na kuboresha afya za wananchi kwa kuhakikisha wanapata elimu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Akizungumza wakati wa uuzaji wa majiko hayo, msimamizi wa mradi kutoka REA Abdulrazack Mkomi amesema serikali imewekea ruzuku ya asilimia 80 katika kila jiko ili kumpunguzia mwananchi gharama, hivyo atanunua jiko kwa Tsh 11,200 badala ya Tsh 56,000.

Aidha, mradi huu unakuja kubadilisha mtazamo wa wananchi katika matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kutoka kutumia kuni na mkaa mwingi hadi kutumia kidogo wakati wa kupika, kwani majiko yametengenezwa kwa nyenzo zinazohifadhi joto kwa muda mrefu na hivyo kupunguza matumizi makubwa ya mkaa na kuni.
Majiko haya hayatoi moshi na hivyo kupunguza uzalishaji wa sumu itokanayo na kuni na mkaa ambayo husababisha magonjwa yanayochangiwa na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba.








