Home Kitaifa RC SENYAMULE ATAKA UWAJIBIKAJI KWA MAAFISA MAENDELEO MKOA WA DODOMA.

RC SENYAMULE ATAKA UWAJIBIKAJI KWA MAAFISA MAENDELEO MKOA WA DODOMA.

Na Deborah Lemmubi-Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule amesema kuwa Maafisa Maendeleo wa Jamii ndio wanaopaswa kuikumbusha jamii wajibu wao pamoja na kuwapa hamasa ya kujiletea Maendeleo kwani wao ni kiungo muhimu cha Maendeleo katika jamii.

Mhe Senyamule ameyaeleza hayo Jijini Dodoma November 18,2025 wakati akifungua Kikao kazi cha Maafisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Dodoma kilichofanyika katika Ofisi yake.

Na kuongeza kuwa ili wananchi wajiletee Maendeleo lazima Maafisa hao wawakumbushe hasa katika kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo fursa za miradi inayotekelezwa.

Sisi Maendeleo ya Jamii tuwe wa kwanza kukumbusha jamii wajibu wao na kuwapa hamasa ya kujiletea Maendeleo,kwani Maendeleo ya Jamii ni kiungo muhimu katika kuleta mabadiliko na Maendeleo na ili wananchi wajiletee Maendeleo lazima afisa awakumbushe hata katika kutumia rasilimali zilizopo kujiletea Maendeleo pamoja na fursa za miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao

Aidha amesema kuwa kwa kuwepo kwao anategemea kuona mabadiliko katika sekta hiyo na kila mmoja atumize wajibu wake kwa kuonesha vitendo kwani inasikitisha kuona wataalam ambao hawapendi fani zao walizosomea wakati wakiwa tayari wameajiriwa,mfano Maafisa misitu,Walimu, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa wa Ardhi na wengineo kuona Mazingira yao yanaharibika na wao wakiwepo hapo.

Naye mmoja wa washiriki wa kikao kazi hicho Bwana Patrick Sebyiga ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Jiji la Dodoma amesema kuwa Maafisa hao ndio chachu ya maendeleo katika jamii hivyo watasimama katika nafasi zao kuhakikisha wananchi wanapata Maendeleo pamoja na kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa na Mkuu wa Mkoa.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Vijijini Bi Elizabeth Shoo amesema kama kuna mahali walilala usingizi basi wameamka na kutambua thamani yao na watasimama mahali walipo kuleta mabadiliko kwani kada yao inagusa vitu vingi sana.

Kikao Kazi hiki kimehudhuriwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii 115 wa Mkoa wa Dodoma na kimeongozwa na Kaulimbiu isemayo “Elimu,Uhamasishaji na Ushirikishwaji wa Jamii ni Silaha za Maendeleo Endelevu“.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!