
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kisarawe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Seleman Jafo, amewataka wananchi wa jimbo hilo kumpa kura za ndiyo ili aendelee kulitumikia na kuliletea maendeleo zaidi.
Akizungumza Septemba 06, 2025, katika moja ya mikutano yake ya kampeni, Dkt. Jafo alisema amefanikisha kukamilisha miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa na mtangulizi wake, ikiwemo ya miundombinu ya barabara, sekta ya elimu, afya, maji na umeme vijijini.
Aidha, Dkt. Jafo alisisitiza mchango wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kusukuma miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR) na Mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ambayo kwa pamoja yanaimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na kuboresha miundombinu ya usafirishaji nchini.








