
Na Deborah Lemmubi-Dodoma.
MTENDAJI Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania Bi Nyakaho Mahemba amesema kuwa Falsafa ya 4R za Dkt Samia kwa ujumla zimewezesha Wasanii kuweza kupata mikopo kwa masharti rahisi na kuanzisha au kukuza miradi Sanaa.
Bi Nyakaho ameyasema hayo mapema Leo hii Jijini Dodoma Februari 28,2025 wakati akizungumza na Wanahabari kuelezea mafanikio ya Mfuko huo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Na kuongeza kuwa Serikali imejizatiti kutoa rasilimali za kifedha na vifaa muhimu kwa wasanii ili kuboresha ubora wa kazi zao na kwamba mikopo hii itakuwa endelevu ili wa sanii waweze kufanikiwa kwa kipindi kirefu na si kwa kipindi kifupi pekee.
“Falsafa ya 4R kwa ujumla ndiyo imewezesha mengi katika mfuko kwani wasani wameweza kupata mikopo kwa masharti rahisi na kuanzisha au kukuza miradi ya Sanaa,na hivyo kuongeza uwezo wao wa kurejesha mikopo kwa ufanisi”.
“Na pia Serikali imejizatiti kutoa rasilimali za kifedha na vifaa muhimu kwa wasanii ili kuboresha ubora wa kazi zao”.
“Kuhusu uendelevu Mikopo imetolewa kwa kuzingatia kwa kuzingatia kwamba msaada huu utakuwa endelevu ili wasanii waweze kufanikiwa katika kipindi kirefu na sio kwa muda mfupi pekee”.
Aidha amesema kuwa Ushirikiano kati ya Serikali,Wasanii na Wadau wa sekta ya Utamaduni ujenga mifumo bora ya usimamizi wa mikopo na maendeleo ya Sanaa,kama vile mashirikano na Taasisi za Kifedha na maonesho ya Sanaa.
Pamoja na hayo ameleeza kuwa Katika mwaka ujao wa fedha 2025/26, Mfuko wa Utamaduni na Sanaa umejipanga kuzidisha ubora na ufanisi wa utoaji wa huduma kwa walengwa pamoja na kushirikiana na wadau katika kutatua kero na changamoto za walengwa ili kuhakikisha wasanii wananufaika na Mfuko huo kama ilivyokusudiwa.
Bi. Nyakaho amefafanua kuwa, ushirikiano na wadau unafanyika ikiwa ni utekelezaji maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufanya kazi na wadau hasa walio katika sekta binafsi.
“Mfuko pia umejipanga kuwezesha wasanii wadogo, wachanga na chipukizi kupitia utoaji wa ruzuku ili kuwawezesha kukuza na kuendeleza vipaji vyao na kuwapa nafasi ya kufanya kazi nzuri katika Sanaa na Utamaduni hasa wakati ambapo hawana uwezo wa kifedha wa kufadhili miradi yao”.
Mfuko wa Utamaduni na Sanaa umeanzishwa kwa Sheria ya Ujumuisho wa Wadhamini na kuanza kutekeleza majukumu yake mnamo mwezi Desemba 2022 huku lengo kuu likiwa ni kuinua ubora wa kazi za Utamaduni na Sanaa ili ziweze kujiendesha kibiashara, kuzalisha ajira pamoja na kuchangia katika pato la Taifa.
