Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imeshiriki katika Maonesho ya Tisa ya Kimataifa ya Uagizaji wa Bidhaa ya China (CIIE) jijini Shanghai, nchini China, kwa lengo la kutangaza Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuwaunganisha wanunuzi wa kimataifa na fursa za biashara ya mazao ya Tanzania.
Katika maonesho hayo ya siku tano (Novemba 5-10, 2026), WRRB imeeleza jinsi mfumo huo unavyowezesha uhifadhi wa mazao katika maghala yenye leseni, utunzaji wa ubora wake na uuzaji wake kwa uwazi.
Akizungumza alipotembelea banda la Tanzania katika maonesho hayo, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shabaan, amepongeza ushiriki wa Tanzania, hususan wa taasisi za serikali, akisema maonesho hayo yanazipa taasisi hizo fursa ya kutangaza huduma zinazotolewa nchini.
Amesisitiza umuhimu wa Tanzania kutumia maonesho hayo kujitangaza kimkakati na kufikia wanunuzi wa kimataifa wanaotafuta bidhaa za Tanzania.
Aidha, Mwakilishi wa kampuni ya Chengdu Jintao Yunhui International Trade Co., Ltd. ameonesha kuvutiwa na ufuta mweupe wa Tanzania, ambao ni miongoni mwa mazao yanayouzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.












