KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga,akizungumza leo Oktoba mosi, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Jukwaa la Wahariri na Wanahabari likiwa na lengo la kuongeza uhabarishaji na uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya nyumba na maendeleo ya makazi.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha mwanzo mpya wa ushirikiano na vyombo vya habari kwa lengo la kuongeza uhabarishaji na uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya nyumba na maendeleo ya makazi, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakipewa nafasi ndogo ikilinganishwa na masuala ya ardhi.
Hayo yamesemwa leo Oktoba mosi, 2026 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga,wakati akifungua Jukwaa la Wahariri na Wanahabari kuhusu Maendeleo ya Makazi , akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia wanahabari kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu fursa, changamoto na suluhisho zinazohusu sekta ya nyumba na makazi.
Amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zenye kina kuhusu mipango ya matumizi ya ardhi, upatikanaji wa makazi bora na usimamizi wa maendeleo ya miji, hatua itakayosaidia jamii kuelewa fursa zilizopo na kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
“Ukuaji wa miji nchini unaendelea kuongeza fursa za ajira, biashara na uwekezaji, lakini pia unaongeza mahitaji ya ardhi, nyumba, miundombinu na huduma za msingi. Hivyo, ni muhimu kwa wananchi kupata elimu ya kutosha kuhusu mipango ya miji na matumizi sahihi ya ardhi ili maendeleo yanayofanyika yaendane na mahitaji ya jamii.”amesema Mhandisi Sanga
Aidha, amesema ukuaji wa miji unapaswa kuzingatia mipango madhubuti na usimamizi bora wa matumizi ya ardhi ili kuhakikisha makazi yanakuwa salama, yanapatikana kwa gharama nafuu na yanastahimili athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na majanga ya asili.
Katibu Mkuu huyo amesema Wizara inaendelea kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau mbalimbali kuweka mazingira ya kisera na kisheria yatakayowezesha matumizi bora ya ardhi na kuboresha upatikanaji wa makazi, huku akisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kufuatilia na kuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa mipango hiyo.
Amesema jukwaa hilo ni mwanzo wa ushirikiano endelevu kati ya Wizara, wahariri, waandishi wa habari, UN-Habitat na wadau wengine katika kuimarisha mijadala ya kitaifa kuhusu maendeleo ya miji na makazi, pamoja na kuibua mawazo na suluhisho zitakazochangia kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania,Dkt.Mary Kafyome, amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kwenda zaidi ya kuripoti taarifa za ujenzi wa barabara, upimaji wa maeneo na ujenzi wa nyumba, bali vinapaswa kuwasaidia wananchi kuelewa maana ya maendeleo hayo, fursa zinazotokana nayo, changamoto zake na nafasi waliyonayo katika kuchangia maendeleo ya miji na makazi.
Amesema wanahabari wanapaswa kutumia takwimu na taarifa za kitaalamu katika kuibua mijadala yenye tija kuhusu maendeleo ya miji na makazi, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu na vyombo vya habari unaweza kusaidia wananchi kuelewa vizuri mabadiliko yanayofanyika katika maeneo yao na namna yanavyohusiana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Naye Afisa Mkazi wa Shirika la Makazi Duniani nchini Tanzania (UN-Habitat), Grace Lubaale, amesema jukwaa hilo ni mwanzo wa ushirikiano kati ya Serikali, vyombo vya habari na wadau katika kuhakikisha taarifa sahihi, za kuaminika na kwa wakati kuhusu maendeleo ya miji na makazi zinawafikia wananchi.
Lubaale ameipongeza Tanzania kwa kuanzisha Jukwaa la Wanahabari kuhusu Maendeleo ya Miji, akisema linaweza kuwa sehemu muhimu ya kuimarisha uwazi, uwajibikaji na uelewa wa umma kuhusu masuala ya makazi na maendeleo endelevu ya miji.
Amesema ushirikiano huo unapaswa kuwa endelevu badala ya kuishia katika tukio moja, ili waandishi wa habari waendelee kupata taarifa na maarifa yatakayowawezesha kuandika habari zenye kina na kusaidia wananchi pamoja na wadau mbalimbali kutoa mrejesho kuhusu changamoto na fursa zilizopo.
Tanzania inatarajiwa kuadhimisha Siku ya Makazi Duniani Oktoba 5, 2026, jijini Dodoma, kwa kaulimbiu “Makazi Toshelevu kwa Wote”, huku Siku ya Miji Duniani ikiadhimishwa Oktoba 31, jijini Dar es Salaam, ikiwa sehemu ya kilele cha maadhimisho ya Urban October.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga,akizungumza leo Oktoba mosi, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Jukwaa la Wahariri na Wanahabari likiwa na lengo la kuongeza uhabarishaji na uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya nyumba na maendeleo ya makazi.


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga,akizungumza leo Oktoba mosi, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Jukwaa la Wahariri na Wanahabari likiwa na lengo la kuongeza uhabarishaji na uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya nyumba na maendeleo ya makazi.

MKURUGENZI Idara ya Maendeleo ya Makazi,Bw.Deogratius Kalimenze,akitoa mada kuhusu Sera ya Makazi na Utekelezaji wake kwa kuzingatia Diara ya Taifa ya Maendeleo 205o wakati wa semina ya Jukwaa la Wahariri na Wanahabari lililofanyika leo Oktoba Mosi 2026 jijini Dodoma.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania,Dkt.Mary Kafyome,akielezea Mafanikio,Changamoto na Fursa za Kuandika ukuaji na Maendeleo ya Miji kwa kuzingatia Diara ya Taifa ya Maendeleo 205o wakati wa semina ya Jukwaa la Wahariri na Wanahabari lililofanyika leo Oktoba Mosi 2026 jijini Dodoma.

Afisa Mkazi wa Shirika la Makazi Duniani nchini Tanzania (UN-Habitat), Grace Lubaale,akizungumza wakati wa semina ya Jukwaa la Wahariri na Wanahabari lililofanyika leo Oktoba Mosi 2026 jijini Dodoma.






























