
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesisitiza umuhimu wa taasisi zilizo chini ya Wizara yake kufanya tathmini za mara kwa mara kama njia ya kuboresha utendaji kazi, kuongeza ufanisi na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kapinga ameyasema hayo Januari 9, 2026 Jijini Arusha wakati wa ufungaji wa Kikao Kazi cha Menejimenti ya Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo, ambapo amesema maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha taasisi zote zinafanyiwa tathmini za mara kwa mara ili kubaini changamoto, kuboresha mifumo ya utendaji na kuongeza uwajibikaji.

Ameeleza kuwa mpango wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaonesha asilimia 22 ya fedha za utekelezaji zitatoka serikalini, asilimia 8 kutoka mashirika ya umma, huku asilimia 70 ikitarajiwa kutoka sekta binafsi. Kutokana na hali hiyo, amezitaka taasisi zenye viashiria vya kujitegemea kupunguza utegemezi kwa serikali na kuongeza ubunifu pamoja na ufanisi katika utoaji wa huduma.
Aidha, Waziri Kapinga amezielekeza taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake kuhakikisha ndani ya siku 100 zinakuwa na mifumo rafiki ya kupokea, kushughulikia na kutoa mrejesho wa changamoto kutoka kwa wananchi na wadau, hatua itakayoongeza uwazi na kuimarisha imani kwa taasisi za umma.

Katika kuongeza ajira na tija, amesema Wizara itaendelea kutegemea Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) katika matumizi ya teknolojia zinazohusiana na mazao ya kimkakati kwa kuzingatia mkoa husika, hatua itakayochochea ajira kwa vijana. Aidha, amewataka Wakala wa Vipimo (WMA) kushuka chini kuwasaidia wananchi kuongeza thamani na vipato vyao, akisisitiza kuwa jukumu hilo lisiachwe kufanywa na taasisi nyingine.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amesema kikao hicho ni muhimu kwa viongozi kwani kinawajengea uwezo kuhusu maadili ya utumishi wa umma, nidhamu, uongozi na afya ya akili, ikiwa ni sehemu ya maono ya Waziri katika kuimarisha utendaji kazi wenye tija ndani ya Wizara.








