
Na Magrethy Katengu – Mzawa Media, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kwa tuhuma za kuendesha televisheni mtandao bila kuwa na leseni. Tukio hili limefanyika kuanzia Oktoba 3 hadi 10, 2025.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Japhet Alex Thobias mkazi wa Sabasaba Ukonga, Joseph Augustino Mabwe mkazi wa Sabasaba Ukonga, wanaodaiwa kumiliki WISPOTI TV, Tegemeo Zacharia Mwenegoha mkazi wa Tabata Ilala, mmiliki wa T.MEDIA TWO, na Elia Costantino Pius mkazi wa Mbezi Juu Kinondoni, mmiliki wa COSTA TV.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 15, 2025, Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alisema upelelezi umekamilika na hatua za kisheria zitachukuliwa ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani haraka kadri itakavyowezekana.
Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa wananchi wanaendelea kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, na halitasita kuwakamata wote wanaotuhumiwa kutenda makosa. Aidha, Jeshi hilo limejidhatiti kuhakikisha hali ya usalama imara ifikapo Oktoba 29 mwaka huu, siku ya Uchaguzi Mkuu, huku likiwahimiza wananchi kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa kwenda kupiga kura kwa amani.