
Na Boniface Gideon, TANGA
Taasisi ya Watoto Foundation yenye makao yake jijini Dar es Salaam, imesema imeanza kutekeleza mradi wake mpya wa Soma na Mama, kwa kugawa vifaa mbalimbali vya elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Ally Yakub Pingizi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa:
Madhumuni ya Daftari la Mama Soma na Samia yanalenga kupitia, yanalenga kuwahamasisha wanafunzi nchini hususan mabinti kusoma kwa bidii na kupunguza utoro mashuleni pamoja na kuwaondolea vikwazo vya ukosefu wa madaftari.
“Tunalenga katika kuwasaidia wanafunzi nchini kusoma katika mazingira mazuri na salama pamoja na kuwa na vifaa muhimu vya kusomea na kujifunzia, tunaamini kupitia kampeni hii itasaidia sana kuwahamasisha wanafunzi kusoma kwa bidii na kufaulu vizuri kwa kiwango cha juu,” alibainisha Ally.
Ally alisema katika programu hiyo wanatarajia kugawa bure madaftari kwa wanafunzi wote, lakini pia watasaidia kutatua changamoto za miundombinu ya shule husika endapo itakuwa na changamoto yoyote.
“Tunatarajia kugawa bure madaftari kwa wanafunzi pamoja na vifaa mbalimbali vya elimu, tumekuja Tanga ambapo tutagawa madaftari kwa shule zote za msingi na tutaendelea kufanya hivyo katika mikoa mingine nchini. Tuwaombe wazazi na walezi watuunge mkono kwenye kampeni hii kwa kuhakikisha watoto wanakuwa na mahudhurio mazuri ya shule ili kwa pamoja tuweze kufikia lengo la watoto wetu kupata elimu bora,” alisisitiza Ally.








