
Sekta ya Viwanda nchini Tanzania imeendelea kutoa majawabu ya fursa za ajira. Hii ni kutokana na nia ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya uanzishwaji wa viwanda ili viweze kuajiri vijana wengi wa Kitanzania kwa lengo la kujipatia kipato.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb) wakati wa uzinduzi rasmi wa kiwanda cha Afriport Apparel Limited Februari 6, 2026 jijini Dar es Salaam.

Londo ameongeza kuwa uwekezaji huo ni ushahidi wa dhahiri wa imani kubwa waliyonayo wawekezaji wa kimataifa kwa Tanzania na mafanikio ya sera na mikakati ya Serikali ya kukuza uchumi wa viwanda.
Aidha, Serikali imeendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji kupitia maboresho ya sera, miundombinu pamoja na urahisishaji wa taratibu za biashara ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha uzalishaji wa Biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mheshimiwa Londo ameongeza kuwa uwekezaji huo unaendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 kwa kukuza sekta ya viwanda, kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kuchochea uhamishaji wa teknolojia na ujuzi kwa Watanzania.
Kwa upande wake, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan, ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuvutia uwekezaji na kukuza sekta mbalimbali za uchumi. Amesema Tanzania inaendelea kujijengea sifa nzuri kimataifa kama eneo salama na lenye fursa nyingi za uwekezaji.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya PORTWEST ambayo ni kampuni kongwe kutoka nchini Ireland, Harry Hughes, ameonesha furaha na kuridhishwa na hatua hiyo ya kimkakati ya uwekezaji, akibainisha kuwa kampuni hiyo imevutiwa na utulivu wa kisiasa, mazingira rafiki ya biashara pamoja na nguvu kazi yenye ari na uwezo mkubwa iliyopo nchini Tanzania.
Ameahidi kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha kiwanda hicho kinazalisha bidhaa zenye viwango vya kimataifa na kuchangia ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa kiwanda hicho, Anna Lucas, ametangaza uwepo wa fursa mbalimbali za ajira kwa Watanzania, akieleza kuwa pamoja na ajira, kiwanda hicho kitatoa mafunzo ya kitaalamu yatakayowawezesha wafanyakazi kuongeza ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la kimataifa.
Katika nadharia ya kiuchumi, uwekezaji huo unakwenda kuimarisha moja kwa moja taswira ya Tanzania kimataifa kama kitovu cha uwekezaji barani Afrika, jambo linaloweza kuvutia wawekezaji wengine katika sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma.
Uzinduzi wa kiwanda cha Afriport Apparel Limited unaendelea kuonesha mafanikio ya jitihada za Tanzania katika kuvutia uwekezaji mkubwa wa viwanda, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha mchango wa sekta ya uzalishaji katika pato la Taifa.








