Na ZIANA BAKARI
WIZARA ya Afya imewataka wananchi kufuata taratibu na miongozo ya Afya ili kuepuka na magonjwa ya mlipuko ambayo yatawaletea matatizo makubwa endapo hawatajikinga na magonjwa hayo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mratibu wa kukinga na kudhibiti magonjwa hayo, Dk. Joseph Hokororo, alisema jamii yatakiwa kuwa makini na magonjwa ya mlipuko kwa kufuata taratibu husika zinazopaswa kufuatwa.

Aidha, alibainisha kuwa mojawapo ya magonjwa ya mlipuko ni Ugonjwa wa Ebola, kwani ugonjwa huo upo nchini Uganda ambao umefika hadi jiji la Kampala.
“Uhusiano wa Uganda na Tanzania ni mkubwa kijamii na kiuchumi, hivyo tunapaswa tuchukue tahadhari za kutosha kujiunga nao licha ya kuwa hivi sasa tunamshukuru Mungu taarifa tulizopata ugonjwa huu nchini Uganda unapungua.
“Tumejipanga vizuri mipakani kote, kuanzia mipaka ya ardhini, viwanja vya ndege na baharini, lengo kubwa ni kuhakikisha watu wote wanaopita katika mipakani tunapata taarifa zao kwa kuangalia dalili za awali,“alisema.

Pia, alisema kwa watakobainika kuwa na viashiria vya ugonjwa wa Ebola hatua za kwanza zitachukuliwa na hata akiwa nchini wataendelea kumfatilia siku hadi siku kuona kama dalili bado anazo.
Mbali na hayo, alisema katika kipindi cha siku 21 mtu anapokuwa ameambukizwa anaweza kuwa na dalili siku yoyote kuanzia siku ya pili.
“Chanzo cha ugonjwa huu unatoka kwa wanyama, aina ya Popo, nyani na sokwe, ugonjwa huo ukitoka kwa wanyama unaingia kwa binadamu na binadamu wanaanza kuambukizana wenyewe kwa wenyewe kwa kushika vitu,
“Sisi binadamu tunaambukizana kupitia vimiminika vya majimaji vya mwili wa binadamu hasa damu, machozi na mafua, hivyo ni vyema kwetu sote kwa pamoja kujikinga na ugonjwa huu,“alisema Hokororo








