Home Kitaifa WANANCHI WA MARA NA SIMIYU WAMSHUKURU DKT. SAMIA KWA MIRADI YA MAENDELEO

WANANCHI WA MARA NA SIMIYU WAMSHUKURU DKT. SAMIA KWA MIRADI YA MAENDELEO

Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhitimisha Mikutano yake ya Kampeni Mkoani Mara leo Oktoba 10, 2025 kwa kuwa na Mikutano ya hadhara kwenye Wilaya za Butiama na Serengeti na baadae mchana kurejea Bariadi Mjini Mkoani Simiyu kuendelea na mikutano ya Kampeni.

Jana Jioni akiwa Musoma Mjini Mkoani Mara kando ya mengine, Dkt. Samia amewaeleza watanzania kiu yake ya kuendelea kuwawezesha kiuchumi na kijamii kwa kuendelea na ujenzi wa Vituo vya mabasi na masoko ya wafanyabiashara kote nchini chini ya mradi wa uendelezaji Miji Tanzania (TACTIC), akitaja ujenzi huo kama fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kunufaika kiuchumi kwani yatajengwa maeneo ya wao kuweza kufanyia biashara zao ndogondogo.

Amesisitiza pia kuendelea kusimamia kikamilifu mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, kurasimisha biashara ndogo ndogo, kuendelea na utoaji wa ruzuku za mbolea, chanjo na pembejeo za kilimo, akisisitiza pia uanzishaji wa mfuko wa uwezeshaji wafanyabiashara wadogo utakaoanza na mtaji wa Bilioni 200, akiwataka Vijana kujiandaa vyema kutumia fursa hizo ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali kupitia uchaguzi Mkuu ujao.

Dkt. Samia anarejea Mkoa wa Simiyu kwenye Wilaya ya Bariadi mara baada ya kuwa na Mkutano wake wa Kwanza Lamadi, Wilayani Busega jana Oktoba 09, 2025 wakati akielekea Mkoa wa Mara, wananchi wakimshukuru kwa kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, jengo la huduma za dharura, ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi kwenye hospitali ya rufaa Nyaumata pamoja na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji Wilayani humo kutoka asilimia 63 hadi 85.

Aidha wananchi wa Bariadi wanamshukuru pia Dkt. Samia kwa kufikisha umeme kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wa dhahabu wa Nyawam, Halawa, Gasuma na Matongo, ujenzi wa majosho 13 ya mifugo pamoja na ujenzi wa barabara za Kilomita 416 za maeneo mbalimbali ikiwemo Nkololo, Dutwam, Mwamondi, Igegu, Matongo, Gibishi, Halawa, Mgodini, Nyamswa, Gambosi, Kilalo, Mwamlapa, Mwabuya, Nkindwabiye na maeneo mengine ndani ya Wilaya hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!