Home Kitaifa Viwanda vitatu vilivyosimama Uzalishaji vyafufuliwa Mkoa wa Tanga

Viwanda vitatu vilivyosimama Uzalishaji vyafufuliwa Mkoa wa Tanga

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, akitembelea na kusikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Rasilimali Watu wa Kiwanda cha African Harmony, Bw. Ahmed Mustapha, kinachozalisha sabuni ya unga aina ya Foma, alipotembelea kiwanda hicho kilichopo mkoani Tanga, akiwa ameambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Mchatta, tarehe 13 Oktoba 2025. Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kufufua na kuimarisha viwanda katika mkoa huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah akikagua Mashine mpya katika Kiwanda kinachotarajiwa kuanza kazi Mwezi Januari cha Ply and Panel kinachomilikiwa na Bw. Hussen Moor, katika ziara yake ya kutembelea Viwanda hivyo vilivyopo mkoani Tanga, akiwa ameambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Mchatta, tarehe 13 Oktoba 2025.

Viwanda vitatu (3) vilivyosimama uzalishaji kwa sababu mbalimbali vimefufuliwa na vitaanza uzalishaji kamili Januari 2026 baada ya kukamilisha hatua mbalimbali ikiwemo ufungaji wa mitambo katika kipindi cha majaribio ya uzalishaji mwezi Desemba 2025.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, Oktoba 13, 2025, akiwa ameambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Mchatta, pamoja na wataalamu wa serikali wakati wa ziara katika viwanda hivyo jijini Tanga kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa jitihada mbalimbali zinazoendelea katika kufufua viwanda mkoani humo ili kuifanya kuwa Tanga ya viwanda.

Aidha, Dkt. Abdallah ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sera, miongozo na kuwezesha ufufuaji wa viwanda hivyo ambavyo vitaongeza ajira, pato la taifa pamoja na uchumi kwa ujumla.

Viwanda vilivyotembelewa katika ziara hiyo ni Kiwanda cha Unique Steel Rolling kinachozalisha bidhaa za chuma, Kiwanda cha Ply and Panel kinachotengeneza bidhaa za mbao ikiwemo samani na magogo, pamoja na Kiwanda cha African Harmony kinachozalisha bidhaa za sabuni, amesema Dkt. Abdallah.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Mchatta, ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara katika kuhakikisha Mkoa wa Tanga wenye rasilimali nyingi zikiwemo madini pamoja na bandari unakuwa na viwanda vingi vinavyofanya kazi ili kukuza uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa viwanda vya Ply & Panel Limited na Unique Steel Rolling, Bw. Hussein Moor, pamoja na Meneja Rasilimali Watu wa African Harmony, Bw. Ahmed Mtomola, wameishukuru serikali kwa kuwezesha ufufuaji wa viwanda hivyo na kuahidi kuwa viwanda hivyo vitatoa ajira kwa watu wengi vitakapoanza kuzalisha kikamilifu.

Nao wafanyakazi katika Kiwanda cha African Harmony, Bw. Edward Mnzava na Richard Mkama, wamesema wamefurahishwa na hatua ya serikali kuwezesha ufufuaji wa viwanda hivyo vinavyotoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa vijana wa mkoa huo, ambao wengi walikuwa mitaani kwa kukosa ajira.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!