Home Kitaifa USHINDANI WA HAKI WACHOCHEA UBUNIFU SOKONI

USHINDANI WA HAKI WACHOCHEA UBUNIFU SOKONI

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema Tume ya Ushindani (FCC) iendelee na majukumu ya kusimamia ushindani katika kujenga imani ya walaji, kwani sekta ya huduma ndiyo eneo ambalo wananchi hukutana moja kwa moja na serikali.

Londo aliyasema hayo wakati alipotembelea Tume ya Ushindani jijini Dar es Salaam. Amesema kuwa ushindani katika soko hujenga imani ya walaji kupata huduma bora na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Amesema imani ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona Taasisi ya FCC inaendelea kulinda ushindani nchini kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa, ili kuhakikisha walaji wanakuwa wa kwanza kutoa taarifa sahihi kuhusu huduma wanazozipata.

Aidha, amesema kuwa katika kuhakikisha wanalinda masoko ya bidhaa za ndani, ni muhimu kwa kuwa Tanzania inafikiwa na mataifa mbalimbali; hivyo, endapo bidhaa hizo zitakuwa chini ya viwango, nchi inaweza kuathirika na kushindwa kupata fedha za kigeni.

Hata hivyo, amesema kuwa wafanyakazi wa FCC waendelee kutoa huduma bora zitakazochochea uwekezaji wa viwanda, hali itakayosaidia kuendelea kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Amesema kuwa matamanio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona tija inaendelea kuongezeka katika malengo ya kukua kiuchumi na kufikia Dira ya Taifa 2050.

Nina imani na FCC, na Wizara tutaendelea kushirikiana katika kuwafikisha Watanzania kwenye kupata huduma bora katika ushindani wa soko wenye uwazi wa bidhaa za ndani na nje ya nchi,” amesema Londo.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, amesema FCC imejipanga vyema kuendelea kushirikiana katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, ili kuendelea kutoa huduma zenye tija kwa mlaji na Taifa kwa ujumla, hususan katika masuala ya ushindani, udhibiti wa bidhaa bandia na ulinzi wa mlaji kwa lengo la kukuza ustawi wa uchumi jumuishi.

Khadija amesema kuwa katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mamlaka waliyopewa kisheria, Tume ya Ushindani (FCC) hufanya kazi kwa karibu na Wizara ya Viwanda na Biashara, Idara na Taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi, kwa kuzingatia dira na miongozo mbalimbali ya kisera, kitaifa na kimataifa, ili kuhakikisha inatekeleza jukumu lake kama chombo cha usimamizi wa utendaji wa ufanisi wa uchumi wa soko kwa kulinda na kushajiisha uzingatiwaji wa misingi ya ushindani wa haki, kumlinda mlaji na kudhibiti bidhaa bandia katika soko la Tanzania Bara.

Amesema majukumu hayo kwa pamoja yanalenga kulifanya soko kuwa shindani na salama, huku walaji wakijenga uaminifu katika bidhaa zinazoletwa sokoni, na hivyo mazingira ya biashara kuchangia ukuaji endelevu na jumuishi wa uchumi na ustawi wa mtu mmoja mmoja.

Amesema FCC ina jukumu la kusimamia ushindani katika soko la Tanzania Bara kwa kuhakikisha inadhibiti makubaliano yanayofifisha ushindani, matumizi mabaya ya nguvu ya soko na miungano ya kampuni inayolenga kuimarisha hodhi ya soko. Tume imepewa mamlaka ya kisheria ya kufanya uchunguzi endelevu (Inquisitorial Procedure) katika kushughulikia ukiukwaji wa Sheria ya Ushindani, ambapo huweza kutoa maamuzi dhidi ya ukiukwaji huo, ikihusisha pia masuala ya kumlinda mlaji.

Aidha, FCC imepata mafanikio makubwa baada ya Marekebisho ya Sheria ya Ushindani, ambapo sasa Sheria hiyo inaweza kufanya maamuzi dhidi ya ukiukwaji wa mashauri yanayohusiana na masuala ya kumlinda mlaji, badala ya masuala hayo kufanywa na mahakama pekee.

Aidha, amesema majukumu mengine wanayotekeleza ni pamoja na kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara wanaobainika kujihusisha na uingizaji nchini, uuzaji, uzalishaji, usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa bandia.

Amesema FCC inatoa elimu na uraghibishi wa ushindani ili kushajiisha utekelezaji wa Sheria ya Ushindani kwa njia ya mashauriano na maelekezo kwa Taasisi za Umma, bila kutumia taratibu za kisheria zenye adhabu mbalimbali.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu amesema FCC ina jukumu la kumlinda mlaji dhidi ya mbinu na mienendo kandamizi na hadaifu katika soko, na hivyo kutoa elimu kuhusu haki na wajibu wa mlaji kupitia vyombo vya habari, tovuti na mitandao yake ya kijamii, kutathmini na kusajili mikataba ya walaji inayoandaliwa na upande mmoja, pamoja na kushughulikia malalamiko ya walaji wa bidhaa na huduma katika soko.

Amesema FCC imewezesha na kuimarisha uwekezaji baada ya kuongeza kizingiti cha ulazima wa kuiarifu FCC kuhusu kusudio la kuunganisha shughuli za kibiashara kutoka shilingi milioni 800 hadi bilioni 3.5. Hatua hiyo imeziwezesha kampuni za wajasiriamali wadogo na wa kati, ambazo thamani ya jumla ya rasilimali zao haifiki kizingiti cha shilingi bilioni 3.5, kuunganisha shughuli zao za kibiashara bila ulazima wa kuomba kibali kutoka FCC. Kwa hatua hiyo, FCC imewezesha ukuaji wa biashara ndogo na za kati, kukuza mitaji ya SMEs, kuziwezesha kukopesheka na kupata teknolojia zaidi ili kushiriki kikamilifu katika uwekezaji na biashara nchini.

Katika hatua hiyo, miungano ya kampuni inayosimamiwa na FCC imeendelea kuleta faida kubwa katika uchumi wa soko, ikiwemo kukuza mitaji ya kampuni husika, kuingia sokoni kwa wawekezaji wapya, upatikanaji wa teknolojia bora za uzalishaji, kuongezeka kwa uzalishaji na tija, kuwezesha upatikanaji wa chaguo la bidhaa na huduma, pamoja na bidhaa kupatikana kwa bei za ushindani na kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi.

Khadija amesema FCC imesogeza huduma karibu na wananchi kwa kufungua Ofisi za Kanda katika Kanda ya Ziwa (Mwanza), Kanda ya Kaskazini (Arusha) na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), pamoja na Ofisi ya Tanga. Baada ya kufungua ofisi hizo, FCC sasa ina jumla ya ofisi sita, zikiwemo Dar es Salaam na Dodoma. Ofisi hizi zinawezesha usimamizi madhubuti wa Sheria ya Ushindani na Sheria ya Alama za Bidhaa kwa ufanisi zaidi.

Khadija amesema FCC imepata Cheti cha Ithibati ya utoaji wa huduma zenye viwango vya kimataifa (ISO CERTIFIED 9001:2015). Amesema kuwa usimamizi mzuri wa misingi ya ushindani, kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ni jambo linaloangaliwa kwa karibu na kuimarishwa, ili kuwapa wawekezaji imani ya kuwekeza nchini kutokana na FCC kuaminika na kuwa miongoni mwa vyombo vya kusimamia uchumi wa soko kwa kuhakikisha urahisi wa wawekezaji kuingia na kutoka sokoni bila vikwazo, pamoja na kusimamia vyema sheria, taratibu na kanuni za ushindani, ulinzi wa mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia katika soko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!