Home Kimataifa UNCDF YAONESHA NIA YA KUONGEZA USHIRIKIANO WA MAZINGIRA

UNCDF YAONESHA NIA YA KUONGEZA USHIRIKIANO WA MAZINGIRA

Shirika la Maendeleo ya Mfuko wa Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) limekubali kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza Programu ya LoCAL awamu ya pili. Kupitia Programu hiyo Serikali inatekeleza Mradi wa Uhimili na Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi wenye thamani ya dola milioni 11 katika halmashauri 18 Tanzania Bara na Zanzibar.

Hayo yamejiri katika Mkutano wa Uwili kati ya Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi, na Afisa kutoka Shirika la UNCDF, Bw. Damiano Borgogno, pembezoni mwa Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea jijini Belem, Brazil.

Mazungumzo hayo yamefanyika wakati wa Mkutano wa 30 wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaofanyika katika Jiji la Belem nchini Brazil ambako Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki. Halikadhalika, katika mazungumzo yao, Shirika la UNCDF limeonesha nia ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika maeneo mengine yanayohusiana na hifadhi endelevu ya mazingira.

Naibu Katibu Mkuu Mitawi amelishukuru shirika hilo kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika usimamizi wa mazingira hususan kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Amesema Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wadau wa maendeleo nchini lengo likiwa kuhakikisha nchi inapata miradi zaidi na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye maendeleo endelevu katika eneo la mazingira.

Eneo mojawapo la ushirikiano lililotajwa ni la Uchumi wa Buluu, ambalo ni sekta muhimu inayokua kwa kasi na kuchochea uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla endapo rasilimali zake zitatumiwa ipasavyo. Ofisi ya Makamu wa Rais tayari imeanzisha Kitengo maalumu cha kuratibu Uchumi wa Buluu na inaendelea kuratibu na kutekeleza Sera ya Uchumi wa Buluu (2024) na Mkakati wake.

Mkutano wa COP30 umeendelea kuwakutanisha wadau wa maendeleo na viongozi kutoka Serikali ya Tanzania kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo na kutafuta fedha kwa manufaa ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!