
Mradi wa kupeleka umeme wa gridi mkoani Kigoma umeokoa takribani shilingi bilioni 58 zilizokuwa zikitumika kila mwaka kwa ununuzi wa mafuta na matengenezo ya majenereta ya kuzalisha umeme.
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema hayo Machi 6, 2026 baada ya kutembelea miradi ya vituo vya kupoza umeme vya Kidahwe, Kigoma Mjini na kituo cha muda cha Kidahwe mkoani humo.

Amesema Shirika la Umeme Tanzania linastahili pongezi kwa kufikisha umeme wa gridi Kigoma kupitia mradi wa kusafirisha umeme kutoka Nyakanazi hadi Kigoma pamoja na kutumia shilingi bilioni tano za fedha za ndani kukamilisha kituo cha muda cha Kidahwe kinachopeleka umeme wakati ujenzi wa kituo kikubwa ukiendelea.
Ameeleza kuwa kituo kipya cha Kidahwe kitakuwa na uwezo wa megawati 192, hatua itakayoimarisha zaidi upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Kigoma ambao kwa sasa unapata takribani megawati 30.

Ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu na utaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Magharibi, kusaidia uendeshaji wa Standard Gauge Railway pamoja na kuchochea biashara ya umeme na nchi jirani.
Kutokana na upatikanaji wa umeme wa kutosha Kigoma, amewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika mkoa huo huku akiwahimiza wananchi kulinda miundombinu ya umeme, akibainisha kuwa Samia Suluhu Hassan anaendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya nishati nchini.








