

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema ukarabati wa Reli ya TAZARA utaimarisha Ukanda wa Kati na Kusini, na kuchochea biashara kati ya Tanzania, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Bara la Afrika kwa ujumla. Amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa Ukarabati Mkubwa wa Reli ya TAZARA iliyofanyika jijini Lusaka, nchini Zambia.
Amesema ukarabati huo utaongeza mauzo ya bidhaa nje na ndani ya Zambia na Tanzania, na kukuza sekta za kilimo, madini, viwanda, utalii pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi wa ukanda huo. Aidha, alibainisha kuwa wakati reli hiyo ikikarabatiwa, Tanzania inaendelea na maboresho makubwa ya bandari zake, ikiwemo upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam chini ya dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuongeza ufanisi, na kuimarisha muunganiko wa Reli ya Umeme ya Kisasa (SGR) na TAZARA. Vilevile, alieleza kuwa Tanzania itaendelea kuboresha bandari za Tanga, Mtwara na Bagamoyo ili kukidhi viwango vya kimataifa vya usafirishaji kwa nchi za Zambia, SADC na Afrika kwa ujumla.

Halikadhalika, Makamu wa Rais alisema ukarabati wa TAZARA unakuja wakati China ikiibuka kama mdau muhimu wa kukuza uchumi wa kimataifa kupitia mpango wake wa 15 wa Miaka Mitano, jambo linaloiweka China kama mshirika muhimu wa maendeleo. Aliongeza kuwa historia imeonesha kuwa Tanzania, Zambia na China zinaposhikamana, hakuna changamoto inayoshindwa kupatiwa suluhisho. Alisisitiza kuwa kama waasisi wa mataifa hayo waliweza kujenga Reli ya Uhuru, basi kwa uwezo wa sasa, mataifa hayo yataweza kukarabati TAZARA na kuifanya kuwa mfano wa ushirikiano wa karne ya 21.
Mamlaka ya Reli ya Tanzania–Zambia (TAZARA) ni moja ya alama muhimu za urafiki, ushirikiano na matarajio ya pamoja kati ya Tanzania, Zambia na Jamhuri ya Watu wa China. Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860 ikiwa na kilomita 975 upande wa Tanzania na kilomita 885 nchini Zambia—inaunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Kapiri-Mposhi Mpya kwa kutumia mfumo wa Cape Gauge (milimita 1,067).
Uwekezaji katika ukarabati huo utahusisha maboresho makubwa ikiwemo ukarabati wa njia ya reli, stesheni, mifumo ya mawasiliano pamoja na ununuzi wa treni 34, mabehewa 760, makochi 18 na treni 2 kwa ajili ya huduma za abiria. Mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo hadi kufikia tani milioni 2.4 katika mwaka wa tatu wa uendeshaji. Ukarabati huo unatarajiwa kuweka reli katika nafasi ya kuwa njia muhimu ya kikanda inayochochea uwekezaji, biashara, kupunguza gharama za usafirishaji na kukuza ushirikiano wa kikanda. Zaidi ya hapo, mradi huo utaimarisha uhusiano kati ya China, Tanzania na Zambia pamoja na kuendeleza mahusiano kati ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hafla ya uzinduzi huo ilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema, pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Li Qiang. Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Nchimbi, aliambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara; Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Mstaafu Mathew Mkingule; Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Masanja; Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum; pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka serikalini.








