Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua,mbali na changamoto mbalimbali zinazoikabili Dunia.
Dk.Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar,alipozungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini,ikiwa ni muendelezo wa utaratibu aliojipangia wa kukutana na waandishi wa habari kila mwisho wa mwezi na kujibu maswali mbalimbali,tukio hilo linalokwenda sambamba na miaka miwili ya Uongozi wake.
Alisema kukua huko kwa uchumi pia kumechangiwa na kuongezeka kwa makusanyo katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume,akibainisha katika sekta ya utalii imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 6.7 katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Septemba 2022,sambamba na Bodi ya Mapato Zanzibar ikiwa katika kiwango bora cha kukusanya Mapato.
Dk.Mwinyi alisema sekta ya Uwekezaji nayo imepata mafanikio makubwa ,ambapo Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imefanikiwa kusajili miradi 181 yenye thamani ya zaidi ya Dola Bilioni Tatu za Kimarekani,huku wastani wa Wananchi 11,289 wakitarajiwa kupata ajira.
Aidha,Dk.Mwinyi alisema Serikali inakusudia kufanikisha miradi mbalimbali katika kipindi cha Miaka Mitatu ijayo,Ukiwemo mradi wa ujenzi wa Bandari Mangapwani,Ujenzi wa barabara kuu Unguja na Pemba ,Ujenzi wa uwanja wa Ndege Pemba pamoja na ujenzi wa barabara za ndani utakaoanza mwezi Disemba,2022 utakaohusisha Ujenzi wa ‘FLY OVER’ katika maeneo ya Mwanakwerekwe na Round about ya Amani.
Alisema Serikali inatambua kuwepo kwa Mfumuko wa bei za bidhaa na kuathiri maisha ya Wananchi wa kawaida ,na kubainisha kuwa jambo hilo linaikabili dunia nzima ikiwemo nchi zinazoendelea.
Alisema hali hiyo inatokana na kupanda kwa bei za vyakula pamoja na mafuta ,kunatokana na majanga ya kilimwengu na akatumia fursa hiyo kuelezea baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kupunguza makali,ikiwemo Kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma,kuangalia pensheni za wastaafu,kuweka fidia katika mafuta pamoja na kutoa huduma bora Bandarini ili kuharakisha utoaji wa bidhaa.
Vilevile,alisema Serikali inaangalia namna ya kubadili mfumo wa adhabu kwa makosa ya usalama barabarani ya papo kwa papo,kwa kigezo cha kuwa mfumo uliopo hivi sasa sio bora.
Dk.Mwinyi aliwashukuru Wananchi kwa kuendeleza Amani,Umoja na Mshikamano ,jambo lililoiwezesha Serikali kuendeleza malengo yake kwa Maendeleo.