Home Kitaifa TUMEDHAMIRIA KUIPAISHA MPANDA KIMAENDELEO – DKT. SAMIA

TUMEDHAMIRIA KUIPAISHA MPANDA KIMAENDELEO – DKT. SAMIA

Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendeleza kasi ya maendeleo katika Mkoa wa Katavi, hususan katika Manispaa ya Mpanda, kwa kuboresha huduma za afya, elimu, barabara, maji, nishati na biashara, ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo.

Akizungumza na maelfu ya wananchi na wanachama wa CCM katika Viwanja vya Azimio, leo Jumamosi, Oktoba 19, 2025, Dkt. Samia amesema Serikali yake itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo yenye lengo la kuinua hali ya maisha ya wananchi, kuongeza ajira na kuboresha huduma za kijamii.

Amesema kuwa miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ukarabati wa miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa maji, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, ujenzi wa jengo la utawala la ghorofa katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, pamoja na ujenzi wa vituo vitatu vya afya katika kata za Misunkumilo, Kasokola na Magamba.

Dkt. Samia ameongeza kuwa Serikali yake pia imetekeleza ujenzi wa nyumba tano za watumishi wa afya, jengo la wagonjwa mahututi, na jengo la dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, miradi ambayo inalenga kuboresha huduma za afya na kusogeza huduma muhimu za kijamii karibu zaidi na wananchi.

Akizungumzia sekta ya miundombinu, Dkt. Samia amesema Serikali imejenga barabara za lami zenye jumla ya kilomita 50 katika Manispaa na Wilaya ya Mpanda, ikiwemo barabara ya Misunkumilo–Mwamkulu yenye urefu wa kilomita 30, pamoja na madaraja manane ya mawe katika maeneo ya Mlimani City, Kasokola, Manga, na Sungamila.

Vilevile, Serikali imekamilisha ujenzi wa masoko ya kisasa katika maeneo ya Mpanda Hotel, Buzogwe, na Soko Kuu, pamoja na maeneo ya kupumzikia na kuchezea watoto katika mitaa ya Maridadi na Siwezi.

Katika sekta ya elimu, Dkt. Samia amesema Serikali imejenga shule tatu mpya za msingi katika maeneo ya Mpanda Hotel, Mlimani City, na Milupwa, pamoja na shule mbili za sekondari katika Mlimani City na Mwamkulu. Aidha, ujenzi wa madarasa 200 ya shule za msingi, vyumba 30 vya madarasa ya sekondari, maabara sita za sayansi, na mabweni matano ya wanafunzi umekamilika.

Kwa upande wa nishati, mgombea huyo wa urais ameeleza kuwa Serikali imepanua njia ya usafirishaji umeme wa kilovoti 400 kutoka Mbeya hadi Kigoma kupitia Mpanda, na imeunganisha zaidi ya wateja 148,000 kwenye gridi ya taifa, pamoja na vitongoji 402 kupitia Mpango wa Umeme Vijijini (REA).

Dkt. Samia amesema utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Kaliua hadi Mpanda wenye urefu wa kilomita 360 ni kielelezo cha dhamira ya Serikali kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria katika Ukanda wa Magharibi.

Ameongeza kuwa ujenzi wa machinjio ya kisasa, viwanja vya michezo, stendi za mabasi, pamoja na maeneo mapya ya biashara unaendelea, huku Serikali ikitekeleza mradi wa maji wa miji 28 na ujenzi wa miundombinu ya kutibu majitaka katika Manispaa ya Mpanda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!