
Na Magrethy Katengu–Dar es Salaam
Katika kuelekea Siku ya Maadhimisho ya Moyo Duniani, ambayo hufanyika kila mwaka Septemba 29, Shirika la Reli Tanzania (TRC), kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wametangaza ushirikiano maalum utakaowawezesha abiria wanaosafiri na treni ya kisasa (SGR) kati ya Dar es Salaam na Dodoma kupata huduma za uchunguzi na vipimo vya afya ya moyo bila malipo.
Akizungumza katika Stendi ya SGR Magufuli leo Septemba 18, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Masanja Machibya, ameeleza kuwa ushirikiano huo ni mwanzo wa mpango mkubwa zaidi wa kimkakati, ambapo TRC ipo kwenye hatua za usanifu za kutengeneza mabehewa maalum yatakayokuwa na vifaa vya matibabu na vitanda, gari la kubebea wagonjwa (“ambulance treni”) ili kuwasafirisha wagonjwa mahututi na wanaopewa rufaa kutoka mikoani kuja Hospitali ya Muhimbili kwa haraka na usalama zaidi.
“Mabehewa haya yatasaidia sana kupunguza muda wa kusafirisha wagonjwa waliopo kwenye hali mbaya kutoka mikoani kama Dodoma na Morogoro kuja Hospitali kubwa ya Muhimbili, kulinganisha na kutumia magari ya dharura (ambulance) ya barabarani. Mpango huu wa mabehewa ya matibabu unatarajiwa kuanza kufanya kazi ndani ya miezi sita ijayo,” amesema Machibya.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, ameeleza kuwa kuanzia tarehe 21 hadi 27 Septemba, wataalamu na mabingwa wa afya watakuwa wakisafiri ndani ya treni ya SGR ili kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na mengine yasiyo ya kuambukiza kwa abiria wote watakaopenda kupima.
Dkt. Kisenge amebainisha kuwa huduma hizo zitatolewa bure kuelekea maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani inayofanyika kila mwaka tarehe 29 Septemba.
“Vipimo hivi vyote, vikiwemo Echo, ECG, vipimo vya sukari na mafuta kwenye damu, vikitolewa hospitalini vinaweza kugharimu zaidi ya Shilingi 500,000, lakini kwa kipindi hiki chote cha wiki ya afya ya moyo, abiria wote watapata huduma hizi bure kabisa wakiwa safarini,” amesema Dkt. Kisenge.
Viongozi hao wametoa wito kwa wananchi na abiria wote wanaosafiri na SGR katika wiki hiyo kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo kupima na kuchunguza afya zao.









