Home Kitaifa SERIKALI YAITAKA SEKTA BINAFSI KUTUMIA FURSA YA MTAJI KUCHOCHEA UCHUMI

SERIKALI YAITAKA SEKTA BINAFSI KUTUMIA FURSA YA MTAJI KUCHOCHEA UCHUMI

Serikali imewataka wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi za fedha nchini kutumia fursa zilizopo katika uchumi wa Tanzania kuwekeza mitaji katika sekta za uzalishaji, miundombinu, teknolojia na biashara ili kuongeza ajira, uzalishaji na ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alipokuwa akizungumza katika Jukwaa la Viongozi wakuu wa Makampuni Binafsi (The 200 CEOs Business Forum Fouth Edition), uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam, ambapo amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji maamuzi madhubuti ya uwekezaji kutoka serikalini na sekta binafsi.

Mhe. Munde alisema Tanzania inalenga kujenga uchumi jumuishi, wenye ustawi, haki na kujitegemea, unaoongozwa na sekta binafsi na wenye ushindani, huku ikilenga kufikia uchumi wa takribani dola za Marekani trilioni moja na kipato cha wastani cha zaidi ya dola za Marekani 7,000 kwa mtu kwa mwaka ifikapo mwaka 2050.

Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, unaenda sambamba na Mpango wa Muda Mrefu wa Maendeleo wa 2026/27–2050/51 pamoja na mipango ya miaka mitano ya maendeleo, ikiwemo Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) wa 2026/27–2030/31, ambapo msingi muhimu wa utekelezaji wa mipango hii ni mfumo wa uwekezaji wa asilimia 70 kwa asilimia 30, na sekta binafsi inatarajiwa kuchangia sehemu kubwa ya uwekezaji huku Serikali tukiendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kisheria, kitaasisi na kiuchumi” alisema Mhe. Munde.

Alisema kuwa, pamoja na umuhimu wa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) kutokana na mchango wake katika kuleta mitaji, teknolojia, utaalamu na fursa za masoko ya kimataifa, Serikali pia inalenga kuwawezesha Watanzania kushiriki zaidi katika uwekezaji ndani ya nchi na itaendelea kuunga mkono ushiriki mpana katika hati fungani za Serikali, mifuko ya uwekezaji wa pamoja, dhamana za kampuni pamoja na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Mhe. Munde aliwataka viongozi wa kampuni, wawekezaji na taasisi za fedha kutumia fursa hiyo ya mitaji kwa kuwekeza katika sekta zinazoongeza uzalishaji na thamani ya uchumi.

Nawataka kuelekeza mitaji katika sekta za uzalishaji, kujenga minyororo imara ya thamani ndani ya nchi na ukanda wa Afrika Mashariki, kutumia teknolojia na akili unde (Artificial Intelligence) kwa uwajibikaji, kuwekeza katika ujuzi na ubunifu pamoja na kujenga kampuni za Kitanzania zinazoweza kushindana katika masoko ya Afrika na dunia” alisema Mhe. Munde.

Aidha aliwahakikishia Serikali iko tayari kusikiliza, kushirikiana na kuendelea kuboresha mazingira ambayo biashara zinaweza kustawi, na mabadiliko yanayolengwa kupitia Dira ya Taifa 2050 yatategemea ubora wa maamuzi yanayofanywa na muhimu zaidi uwezo wa kuyageuza maamuzi hayo kuwa uwekezaji, uzalishaji, ajira na ustawi wa pamoja.

Alisema kuwa Serikali imeendelea kutekeleza mageuzi ya kiuchumi, kisheria, kitaasisi na kiutawala yenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ambapo awamu ya kwanza ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI I) iliyoanzishwa mwaka 2018, ilisaidia kurahisisha taratibu za biashara, kuimarisha huduma kwa wawekezaji na kupunguza vikwazo vya udhibiti, huku ikiendelea na awamu nyingine ya mageuzi hayo ili kukidhi mahitaji ya sasa ya kiuchumi, kiteknolojia na kibiashara.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya, alisema kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kupitia sera zake ili kupata vyanzo mbalimbali vya fedha kwa ajili ya kukuza na kupanua biashara zao.

Mhe. Chaya alisema kuwa, Serikali inahitaji kuona biashara zikikua kutoka ndogo kuwa za kati, kutoka za kati kuwa kampuni kubwa, na hatimaye kutoka kampuni zinazofanya kazi ndani ya nchi kuwa kampuni imara zinazoweza kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Alisisitiza kuwa Serikali ina jukumu la kuweka mazingira wezeshi, huku sekta binafsi ikiwa na wajibu wa kujenga taasisi imara, kuimarisha utawala bora wa kampuni, kuwekeza katika watu na teknolojia, na kujenga biashara zenye uwezo wa kushindana nje ya mipaka ya Tanzania.

Tanzania iko katika nafasi nzuri kunufaika kutokana na utulivu wa kisiasa, jiografia yake ya kimkakati, rasilimali za asili, ongezeko la idadi ya vijana, maboresho ya miundombinu pamoja na fursa zinazotokana na masoko ya kikanda na bara” alisema Mhe. Dkt. Chaya

Aidha, aliitaka sekta binafsi kutumia fursa hizo kwa kuangalia zaidi ya soko la ndani, huku Serikali ikiendelea kushirikiana na wafanyabiashara kubaini na kuondoa changamoto zinazokwamisha uwekezaji na ukuaji wa biashara.

majukwaa kama haya yanapaswa kwenda zaidi ya kuwa sehemu za mazungumzo na kujenga mitandao, bali yazalishe matokeo yanayoonekana katika uchumi, ikiwemo kuunganisha mtaji na fursa halisi za uwekezaji, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi na kubaini vikwazo vinavyoathiri uwekezaji na ukuaji wa biashara” alisema Mhe. Dkt. Chaya

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!