Home Kitaifa TBS MWENYEJI WA KIKAO CHA KIMATAIFA CHA VIWANGO VYA NAFAKA , OKTOBA...

TBS MWENYEJI WA KIKAO CHA KIMATAIFA CHA VIWANGO VYA NAFAKA , OKTOBA 20 – 21, 2026 DAR ES SALAAM .

Na Mwandishi Wetu.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linatarajia kuwa mwenyeji wa kikao cha Kamati ya Wataalamu wa Kimataifa ya uandaaji wa viwango vya nafaka na mazao ya jamii ya kunde, kitakachofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 20 na 21, 2026.

Akizungumza kuhusu kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa kikao hicho kinachoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO), ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kupokea mkutano wa kamati hiyo ya wataalamu.

Amesema fursa hiyo itaitangaza Tanzania kimataifa na kuwawezesha wataalamu wa ndani kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa viwango vya kimataifa vya nafaka na mazao ya jamii ya kunde kupitia Kamati ya ISO/TC 34.

Dkt. Katunzi amesema kikao hicho kinatarajiwa kushirikisha wataalamu kutoka maeneo mbalimbali duniani, pamoja na wadau wa kitaifa watakaotoa mawazo, uzoefu na utaalamu wao katika kuboresha uandaaji wa viwango vya mazao hayo.

Amesisitiza kuwa TBS itaendelea kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika uandaaji na utekelezaji wa viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuongeza imani ya watumiaji kwa bidhaa na huduma, kuchochea ubunifu na ushindani, kuongeza tija na kuwezesha biashara za ndani na kimataifa.

Ameongeza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mchango wa TBS katika kufikia malengo ya maendeleo ya muda mfupi na mrefu, hususan yale yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Aidha, Dkt. Katunzi ametoa shukrani kwa ISO kwa kukubali wataalamu na wajumbe wa kamati hiyo kushiriki katika uandaaji wa viwango nchini Tanzania, huku akiwakaribisha wadau wote wa nafaka na mazao ya jamii ya kunde kushiriki katika kikao hicho ili kuchangia mawazo na utaalamu wao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!