Home Kitaifa TAHILISO YAPAZA SAUTI: VYUO VITOE AVN KWA WAKATI

TAHILISO YAPAZA SAUTI: VYUO VITOE AVN KWA WAKATI

Magrethy Katengu —Mzawa media Dar es Salaam

Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHILISO) amewataka watendaji wa vyuo vya elimu ya juu kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza ngazi ya stashahada (diploma) wanapatiwa namba za uthibitisho wa sifa za kujiunga na shahada (AVN) kwa wakati ili kuwawezesha kuendelea na masomo bila vikwazo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 20,2026 jijini Dar es Salaam, Rais huyo amesema TAHILISO inasikitishwa na ucheleweshaji wa namba hizo, ambao umekuwa ukisababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kujiunga na masomo ya shahada kwa wakati, licha ya kutimiza masharti yanayotakiwa.

Amesema hali hiyo inaweza kudhoofisha juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu ya juu, ikiwemo kuongeza uwekezaji katika mikopo ya ada na fedha za kujikimu, kujenga kampasi za vyuo katika mikoa mbalimbali, kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kujenga hosteli za wanafunzi.

“Naiomba taasisi na watendaji wa vyuo husika kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto za wanafunzi waliokwama kupata namba hizo. Jukumu hili ni la vyuo na watumishi wenye dhamana, hivyo halipaswi kuachiwa wanafunzi kubeba mzigo huo,” amesema.

Katika hatua nyingine, amezitaka taasisi zinazohusika na huduma za bima ya afya kwa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu kutatua changamoto zinazohusiana na ucheleweshaji wa bima, kutokuwepo kwa uelewa wa kiasi cha malipo kinachotakiwa pamoja na mifumo ya kielektroniki kutokusomana.

Amesema changamoto hizo zimekuwa zikilalamikiwa na wanafunzi na wakati mwingine kuwafanya washindwe kupata huduma za afya wanapozihitaji, hali inayoweza kuathiri ustawi wao na mwendelezo wa masomo.

Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa Mkurugenzi wa Bima ya Afya na wasaidizi wake kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili wanafunzi waweze kupata huduma kwa wakati na kwa utaratibu unaoeleweka.

Aidha, amewaomba wamiliki wa nyumba na hosteli zinazopangishwa kwa wanafunzi kuzingatia hali ya kiuchumi ya vijana hao na kuepuka kuongeza kodi kwa viwango vinavyowaongezea mzigo wa gharama za maisha.

Amesema baadhi ya wamiliki wamekuwa wakipandisha kodi ya nyumba kutoka Sh70,000 hadi Sh100,000, hatua ambayo amesema inawaweka wanafunzi katika mazingira magumu ya kifedha, hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao hawana vyanzo rasmi vya mapato.

Ameeleza kuwa baadhi ya wanafunzi hutegemea michango ya wazazi, walezi, ndugu na marafiki ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku wanapokuwa vyuoni. Wengine wanatoka katika familia ambazo zimeamua kuuza mali, ikiwemo mifugo na mashamba, ili kupata fedha za kugharamia elimu ya watoto wao.

Kwa msingi huo, amewasihi wamiliki wa nyumba na hosteli kuwa na huruma na kuweka viwango vya kodi vinavyozingatia uwezo wa wanafunzi, ili kuwawezesha kuishi katika mazingira mazuri na kuendelea na masomo yao bila kukabiliwa na changamoto kubwa za makazi.

Amesisitiza kuwa ustawi wa wanafunzi wa elimu ya juu unapaswa kupewa kipaumbele kwa kushughulikia changamoto zinazowakabili katika masomo, huduma za afya na makazi.

Amesema ameamua kuanza kwa kuzungumzia changamoto zinazowakabili wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu kabla ya kuingia katika masuala mengine ya kisiasa na yanayohusu hali ya nchi, akieleza kuwa masuala ya elimu na ustawi wa wanafunzi yanahitaji kupewa uzito unaostahili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!