Home Kitaifa SERIKALI YATENGA BILIONI 8 KUSOMESHA WATAALAMU WA AFYA NGAZI YA UBINGWA NA...

SERIKALI YATENGA BILIONI 8 KUSOMESHA WATAALAMU WA AFYA NGAZI YA UBINGWA NA UBINGWA BOBEZI

Na. Catherine Sungura, WAF-Dar es Salaama

Serikali kupitia Wizara ya afya imetenga billion 8 kusomesha watalaamu wa afya, ndani na nje ya nchi, katika fani mbalimbali za kibingwa ikiwemo upasuaji wa watoto.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi mara baada ya kuwajulia hali watoto mapacha (Rehema na Neema) waliokuwa wameungana na kufanikiwa kutengenishwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili mnamo Julai Mosi mwaka huu.

Prof. Makubi amesema kuwa fedha hizo zitawasaidia wataalamu wa afya ili kuweza kujiendeleza kwa ngazi ya kibingwa na ubingwa bobezi na kuwataka Watalaamu kujitokeza.

Ili kuendelea kuboresha huduma za kibingwa nchini tumetenga bilioni 8 za kuwaendeleza wataalamu wetu ndani na nje ya nchi kwa fani mbalimbali ikiwemo upasuaji wa watoto” Amesema Prof. Makubi

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejenga mfumo bora wa vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya wagonjwa mahututi (ICU) kutoka ngazi ya Taifa hadi hospitali za Halmashauri.

Kwa upande wa watoto mapacha waliofanyiwa upasuaji wa kuwatengenisha Prof. Makubi amesema upasuaji huo wa kihistoria kwa watoto hao walioungana tumbo na kifua ni mfumo bora uliowekwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa ngazi zote nchini.

Rais Samia na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wanatoa pongezi kwa wataalamu wetu nchini wakishirikiana na wale wa chuo Kikuu cha Bahrain kwa kufanikisha upasuaji mkubwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili” Aliongeza

Aidha, Prof. Makubi amesema Mapacha hao wanaendelea vizuri chini ya uangalizi maalumu wa wataalamu wa hospitali ya Taifa Muhimbili.

Hata hivyo Prof. Makubi amewatia moyo na kuwashukuru wataalamu wa afya kwa huduma ya upasuaji na kusema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mafunzo,vifaa, vifaa tiba pamoja na miundombinu katika eneo la upasuaji nchini.

Akizungumza kwa mara ya kwanza ,Mama wa pacha hao Bi.Amina Amos amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha wataalamu kufanikisha upasuaji wa pacha wake.

Napenda kushukuru Taifa letu na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwezesha kunitenganishia watoto wangu salama pamoja na Madaktari kutoka nje,nashukuru sana wauguzi hapa PIKU wamenilelea vema watoto wangu hadi sasa

Nimepata changamoto nyingi lakini sasa hivi ninafurahi kwa sababu napata kila mahitaji ya watoto, nimelelewa vizuri pamoja na watoto”.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!