
Na Shomari Binda-Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amewahamasisha wanawake wajasiliamali kukopa mikopo isiyokuwa na riba kutoka kwenye halmashauri.
Kauli hiyo imetolewa leo machi 12,2025 kwa niaba yake na Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Mara Omary Gamuya alipokuwa akifunga kongamano la wanawake wajasiliamali kwenye ukumbi wa uwekezaji.
Amesema hadi sasa kupitia halmashauri zake 9 tayari mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 2 imetolewa kwa makundi ya wanawake,vijana na wenye ulemavu na kuendesha biashara zao.
Mtambi amesema mkoa wa Mara unazo fursa nyingi za biashara ambazo wanawake wajasiliamali wanaweza kuzifanya na suala la mitaji ni vyema kufatilia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
Amesema mikopo ya mitaani yenye riba kubwa imekuwa ikiwarudisha nyuma wanawake wengi na kushauri kuachana nayo kwa kuwa haina faida.

Aidha amesema yapo masoko ya nchi jirani ambayo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira mazuri ya kufanya biashara ambayo yakitumiwa yatainua uchumi wa wanawske wajasiliamali.
Mkuu huyo wa mkoa amelipongeza shirika la Power Life kwa kuandaa kongamano na maonyesho ya biashara kwaajili ya kuwasaidia wanawake wa mkoa wa Mara.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Biashara Gambales Timotheo amewataka wanawake hao wajasiliamali kujiunga na mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa na shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo( SIDO) ili kuongeza thamani ya bidhaa zao.
” Kongamano hili la leo litatufanya tuwe wapya kwenye biashara zetu tunazo zifanya na nishauri kutumia shirika la SIDO ili kupata mafunzo na kuzipa thamani bidhaa zetu”,amesema Gambales.
Mkurugenzi na mwanzilishi wa shirika la Power Life Mariam Suleiman amesema wamefanya makongamano kwenye halmashauri zote za mkoa wa Mara kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kuweza kuwajengea uwezo wanawake kwenye shughuli zao za ujasiliamali.
