
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Petro Magoti, ametoa wito kwa wazazi wote wenye watoto wenye ulemavu kuhakikisha wanawaandikisha shule wanapofikia umri wa kuanza elimu ya awali au darasa la kwanza. Amesema wazazi wasio na uwezo wa kuwapatia watoto wao baiskeli maalum wafike ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili kupatiwa msaada huo.
Ameeleza kuwa dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kuona watoto wote wenye mahitaji maalum wanapata haki yao ya msingi ya elimu bila kikwazo chochote. Ameonya kuwa kuanzia tarehe 13, mzazi yeyote atakayebainika kumzuia mtoto mwenye ulemavu kwenda shule atachukuliwa hatua za kisheria.

Mhe. Magoti amewataka wakazi wa Kisarawe kuacha kuwaficha watoto na kushirikiana na serikali kutatua changamoto zozote zinazokwamisha mahudhurio ya masomo kwa kufika ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ambako watakutana na watendaji wa serikali kwa ajili ya kupanga utaratibu wa mtoto kuanza shule.
Vilevile, ametoa maelekezo kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari kuwapokea wanafunzi wote bila kuwazuia kwa kisingizio cha kukosa sare. Amesisitiza kuwa mwanafunzi aanze masomo mara moja huku mzazi akiendelea na mchakato wa kupata sare, bila kumrudisha mtoto nyumbani kwa sababu hiyo.








